Wauawa baada ya Al-Shabab kuvamia hoteli


Takriban watu saba wameuawa katika shambulio moja la hoteli kusini mwa Somalkia ikiwemo mwandishi wa runinga mwenye uraia wa Canada na Somali Hodan Nalayeh, kulingana na ripoti.

Maafisa na wale walionusurika wanasema kuwa mlipuaji wa kujitolea muhanga aligongesha gari lililojaa vilipuzi katika Hoteli ya Asasey katika bandari ya Kismayo kabla ya washambuliaji hao kuvamia jengo hilo.

Nalayeh na mumewe wameripotiwa kuwa miongoni mwa wale waliouawa. Kundi la wapinganaji la al-Shabab limekiri kutekeleza shambulio hilo.

Walioshuhudia wanasema kuwa walisikia milio ya risasi baada ya bomu lililokuwa ndani ya gari hilo kulipuka.

Haijulikana iwapo washambuliaji hao walisalia ndani ya hoteli hiyo baada ya mlipuko huo.

Afisa wa usalama, Abdi Dhuhul aliambia chombo cha habari cha AFP kwamba waziri mmoja wa utawala wa eneo hilo pamoja na wakili ni miongoni mwa waliofariki.

Vyombo vya habari katika eneo hilo na muungano wa waandishi wa Somali unasema kuwa Nalayeh ,43, pamoja na mumewe ni miongoni mwa wale waliouawa.