Area C United yaanza kwa sare na Fountain, Dodoma Pre - Season Cup


Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma

Timu ya Area C United na Fountain Academy wameanza kwa sare ya kuto kufungana katika mchezo wa kwanza wa mashindano ya Dodoma Pre season Cup yaliyoanza kutimua vumbi katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Mashindano hayo ambayo yameanzishwa rasmi kwa ajili ya kuziandaa timu za Mkoa wa Dodoma zinazojiandaa na mashindano mbalimbali kujinoa kwa ajili ya ligi wanazoshiriki.

Timu zinazoshiriki ligi hiyo ni Dodoma FC inayoshiriki ligi daraja la kwanza Tanzania bara, Fountain Academy, Area C United ambazo zinashiriki ligi daraja la pili na Dodoma Combine inayoshiriki ligi hiyo kuchukua nafasi ya timu ya Mji Mpwapwa ambayo haikushiriki mashindano hayo ya Dodoma Pre season Cup.

Mchezo uliokuwa mkali na wakusisimua kutokana na umahili wa timu zote mbili ulishuhudiwa timu hizo zikitoka sare ya kutokufungana ndani ya dakika zote tisini za mchezo huo.

Mara baada ya mchezo huo Kocha wa Area C United Henry Mkanwa, amesema mashindano hayo ni mazuri kwao kwani watatambua mapungufu ya timu yao na kuyarekebisha kabla ya mashindano.

"Michezo hii itatusaidia Sana kwa sababu itatuonesha mapungufu yaliyopo kabla ya ligi haijaanza na baada ya michezo huo tunatarajia kucheza na Singida United na Lipuli ya Iringa nadhani michezo hii itatupa picha halisi ya timu yetu" amesema Mkanwa.

Kwa upande wake kocha msaidizi wa Fountain Academy Robart Kasiga, amesema watatumia mashindano hayo kujiweka sawa na ligi daraja la pili inayotarajiwa kuanza hizi karibuni.

Mratibu wa mashindano hayo Poul Domician amesema wameandaa mashindano hayo kwa lengo la kuzinoa timu za Mkoa huo kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali yanayowakabili mbeleni.

Amesema lengo la mashindano hayo ni kuzitambulisha timu hizo kwa mashabiki wa mpira Dodoma na kuwaunganisha na kuzishabikia timu hizo ili ziweze kufanya vizuri katika mashindano yanayowakabili.

Amesema wanamalengo ya kuyafanya mashindano hayo kuwa makubwa zaidi na kuanzia mwakani watazialika na timu za nje ya Mkoa wa Dodoma zikiwamo za ligi kuu kuyapa uzito mashindano hayo.