CCM kupambana na wenyeviti watakao poteza mitaa



Na Amiri kilagalila-Njombe

Chama cha mapinduzi CCM mkoa wa Njombe kimeapa kupambana na wenyeviti wa matawi  watakaopoteza ushindi katika uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 11 mwaka huu.

Katibu wa siasa na uenezi mkoa wa Njombe Erasto Ngole wakati akitoa mwelekeo na maelekezo ya chama hicho kwa viongozi wa mashina,matawi na kata katika  ofisi ya CCM  kata ya kitisi mjini Makambako kuelekea uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa,amesema chama hicho hakipo tayari kukaa na viongozi mzigo kwa sasa kwa kuwa kimejipanga kushika dola.

“Sisi kwa upande wetu kwenye vikao vya kimkoa tumeshamaliza tunakwenda kuchukua dola,sasa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wilaya haihusiki,mkoa hausiki na anayehusika ni tawi,mwenyekiti wa tawi,katibu wa tawi,kamati ya tawi pamoja na mabalozi hii ngoma ni yenu,kata wanasubiri uchaguzi wa diwani kila mmoja atabeba mzigo wake”alisema Ngole

Kwa upande wake mwenyekiti wa jumuiya ya vijana UVCCM mkoa wa Njombe Nehemia Tweve ametoa wito kwa vijana kujitokeza katika nafasi hizo huku akiwataka kuwa macho na viongozi wasiofaa katika maeneo yao.

Naye katibu wa siasa na uenezi wilaya ya Njombe Hitler Benjamin Msola ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu litakapofika mkoani Njombe,huku akipendekeza wabunge kubadili katiba ili Rais aweze kuongoza kwa kipindi kirefu.

“kwa kweli kazi za Rais tunaziona katika mkoa wa Njombe,kwanini tusiwe kama China Rais John Magufuli awe wa kudumu,mimi mtu akiniuliza leo mnataka tufanye uchaguzi wa Rais mwakani ningesema huyu Rais aendelee mpaka Mungu atakapo mchukua”alisema Hitler Msola


Katika hatua nyingine katibu wa siasa na uenezi wa chama hicho mkoa wa Njombe Erasto Ngole amefika na kuzungumza na viongozi pamoja na wanachama wa CCM shina namba nne lililopo mtaa wa jogoo mjini hapo na kuwapokea wanachama wapya 17  waliojiunga na chama hicho.