Humphrey Polepole awapa tano UWT


Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Humphrey Polepole amesema chama hicho kinathamini sana mchango mkubwa unaofanywa na UWT katika kukitangaza chama hicho na kuendelea kukubalika ndani na nje ya nchi.

Sambamba na hilo ameitaka jumuiya hiyo(UWT) kuhakikisha inatengeneza kanzi data na kuwa na takwimu za wanachama wa UWT waliona elimu na ujuzi mbalimbali  ili kupata nafasi haraka pindi nafasi zinapohitajika kwa uteuzi.

Polepole ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akifungua baraza la kwanza la UWT taifa kwa mwaka 2019, amesema jumuiya hiyo imekuwa na mchango mkubwa sana katika kikitangaza chama hicho ndani na nje ya nchi.

“Mnafanya kazi kubwa sana jumuiya hii nadhani tungekuwa na wababa tupu nadhani tungekuwa tumeanguka mda mrefu, andaeni kanzi data ambayo itakuwa na takwimu sahihi kwanza wenyewe mjue kuna wanawake wakuu wa Wilaya Mikoa/Wilaya wangapi na pindi nafasi zinapotokea tujue wanaotufaa” amesema Polepole.

Ameeleza chama kina fanya kazi kubwa sana “ukiangalia tangu mwaka 1961 mpaka 2015 tulikuwa na vituo vya afya 115 lakini kwa kasi ya sasa tangu 2017-2019 tumejenga vituo vya afya 355 kote nchini kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya afya” amesema.

Amesema kutokana na uimara wa wanawake katika kukitangaza chama wamepanga kuwaimarisha katika Nyanja za kiuchumi ili wawe na nguvu zaidi kukitangaza chama zaidi kote nchini.

Licha ya kutoa elimu bure kwa ngazi ya msingi mpaka kidato cha nne bado wameanzisha mfumo mwingine wa kutoa elimu ya ufundi stadi bure ili kuweza kuwaokoa watoto ambao hawapo katika mfumo wa elimu lengo ni kuwaokoa na janga la mimba na ndoa za utotoni.

“Tumeanzisha mafunzo hayo kuwa okoa watoto walio nje ya mfumo na niwaambia akina baba mtoto aliyeko katika elimu ya ufundi stadi ni sawa na mwanafunzi adhabu kwa atakaye oa au kusababishia ujauzito adhabu ni zilezile miaka 30 jela” amesema.

Kwa upande wake Katibu mkuu wa UWT taifa Qeen Mlozi, wameendelea kuimarisha chama hicho kuanzia ngazi ya chini mpaka ngazi za juu, na kuhakikisha wanakitangaza chama hicho kikamilifu na kuahidi ushindi wa kishindo katika chaguzi zote zijazo.