Iran yatoa onyo kwa Marekani

Iran imesema leo kuwa imeionya Marekani dhidi ya jaribio la kuikamata meli ya mafuta ambayo imeondoka eneo la Gibraltar, licha ya juhudi za Marekani kuizuia.

Msemaji wa wizara ya masuala ya nje ya Iran, Abbas Mousavi, amewaambia wanahabari kuwa Iran imetoa onyo linalohitajika kwa maafisa wakuu wa Marekani kupitia mifumo yake rasmi kutochukuwa hatua hiyo, maana itakuwa na athari mbaya.

Iran ilikuwa na mzozo wa bahari kuu na Uingereza, tangu jeshi la mshirika huyo wa Marekani kuizuia meli hiyo katika pwani ya Gibraltar, mnamo Julai 4 ikidai ilikuwa inasafarisha mafuta kupeleka nchini Syria na hivyo kukiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya.

Wiki mbili baadaye, Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi wa Iran kiliikamata meli ya Uingereza katika eneo la Ghuba katika kile Uingereza ilichokitaja kuwa hatua ya kulipiza kisasi.

Hata hivyo, hii leo wizara ya mambo ya nje ya Iran imetupilia mbali dhana hiyo kwamba kulikuwa na uhusiano kati ya visa hivyo viwili vya kuzuiliwa kwa meli.