Na Ahmad Mmow, Lindi.
Jeshi la Kujenga Taifa ( JKT) limepata ushindi wa jumla na vyombo vya ulinzi katika maonesho ya Nanenane kanda ya Kusini.
JKT ambayo inashiriki maonesho hayo kila mwaka tangu kuanza kuanza kuoneshwa katika kanda ya Kusini imeendeleza rekodi yake yakuwa mshindi wa jumla. Ambapo tangu yaanze imekuwa kinara kwa kanda hii ya Kusini.
Akizungumza na Muungwana Blog baada ya ushindi huo, mwakilishi wa JKT katika maonesho hayo kwa kanda ya Kusini, Luteni kanali Juma Mrai alisema jeshi hilo huwa linajipanga na kujiandaa kikamilifu kushiriki maonesho hayo na mengine.
Kwani linatambua umuhimu wa maonesho hayo kwa wananchi.
Alibainisha kwamba maonesho ya Nanenane ni muhimu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi kwani yanaweza kuwa natija kwao iwapo watajifunza mambo mbalimbali yanayooneshwa. Kwahiyo wataboresha shughuli zao nakuongeza uzalishaji wa mazao.
Kamanda Mrai alisema licha ya kushiriki maonesho hayo lakini pia linatekeleza kwa vitendo yale yanayooneshwa na jeshi hilo kwenye viwanja vya maonesho.
Katika kuthibitisha hayo, Luteni Kanali Mrai alisema takribani vikosi vyote vina mashamba ya mahindi na viwanda vya kuchakata mahindi.
'' Kwa mfano kikosi cha Mlale pekee kinazalisha tani 308 za sembe kwa mwezi. Kwa siku kinachakata tani 20, kwa mwezi tani 44O. Hiyo ni kwa sekta ya kilimo,'' alisema kamanda Mrai.
Alisema siri ya mafanikio yao ni ushirikiano wanaopata kutoka kwenye taasisi za serikali na wananchi, moyo wa uzalendo, utii, kupokea maelezo na kufanya kazi kwa weledi.
'' Licha ya kuwatayarisha vijana wapate ujuzi katika fani mbalimbali ili waweze kujiajiri, lakini pia jukumu kubwa la JKT nikuwalea nakuwafanya wapende nchi yao na wawe wazalendo. Jukumu ambalo linafanikiwa,''alisema.
Aidha kamanda huyo aliweka wazi kwamba jeshi hilo limepokea kwa mikono miwili na mwitikio mkubwa sera ya kujenga nchi wa kati kupitia viwanda.
