Kilio cha wakulima wa mbaazi chahamia kwa wakulima wa nazi



Na. Ahmad Mmow, Kilwa.

Baadhi ya wakulima wa nazi katika tarafa ya Kipatimu, wilaya ya Kilwa, mkoa wa Lindi wanaiomba serikali iwatafutie soko la zao, kutokana na  kukosa wanunuzi.

Leo, wakizungumza na Muungwana Blog kwanyakati tofauti katika za vijiji vya Namayuni na Chumo walisema nazi zimekosa wanunuzi nakusababisha ziuzwe kwa shilingi 100 kila nazi moja.

Mwananchi, Mshamu Mmondya  alisema nazi ambalo ni zao kuu la  biashara katika maeneo hayo. Hata hivyo mwaka huu bei ya nazi moja haizidi shilingi 150. Hata hivyo wanunuzi hawaonekani.

Alisema msimu huu nitofauti na mwaka jana ambao mwezi kama huu (Agosti) nazi moja iliuzwa na kununuliwa kwa shilingi 400 hadi mia 500. '' Hatujui sababu na tumekwama, serikali itutafutie suluhisho lakudumu la soko la nazi. Nazi ndio zao letu kuu la uchumi, siku za nyuma tulikuwa tunapata fedha kupitia mbaazi. Lakini nalo halina bei na wakulima wengi tumesusa kulima zao hilo,'' alisema Mmondya.

Maelezo ya Mmondya yaliungwa mkono na Zawadi Bungara aliyesema bei ya nazi inasababisha washindwe kumudu kugharama za kambi za watoto wao wa darasa la saba na kidato cha nne.

Zawadi kwa masikitiko makubwa alisema hawajui itakapofika mwezi Januari mwakani maisha yao yatakuwaje na wataishi vipi. Kwamadai kwamba wakati bei ya nazi ikiwa hivyo, lakini bei ya vyakula na bidha nyingine zinapanda siku hadi siku.

Masikitiko na kilio cha bwana Mmondya na Bi Zawadi Bungara kiliungwa mkono na mzee Abdallah Ngalicha. Yeye licha ya kuunga mkono maelezo hayo alishauri kuwepo mpango mahususi wakuliongezea thamani zao hilo kwa kujenga viwanda vidogo vya kukamua mafuta. Akiweka wazi kwamba tatizo la soko lipo katika tarafa yote ya Kipatimu na hata Miteja na Njinjo.

Hata hivyo mtendaji wa kijiji cha Nahama, Lipi Benju, licha ya kukiri kwamba mwaka huu soko la nazi ni gumu alitoa wito kwa wananchi wa kijiji hicho waunge mkono nia ya serikali ya kuwakwamua kiuchumi kwa kuanzisha vikundi vya ujasiriamali na kuanzisha miradi ya kiuchumi.

'' Waunge mkono kwa kuanzisha vikundi vya ujasiriamali ili waweze kukopesheka na kuanzisha viwanda hivyo vidogo. Lakini pia wanaweza kuanzisha kilimo cha mazao mengine mbadala wa nazi na ufugaji kuku hata nyuki. Kwahiyo tunapowahamasisha watusikilize na wafanyie kazi. Nikweli soko la nazi siyo zuri, ila lazima tuchukue hatua  sio kulia tu,'' alisema Benju.