Kujengwa kwa hoteli ya kisasa ya Madinat El Bahr ni hatua kubwa - Dkt. Shein



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa kujengwa kwa hoteli ya kisasa ya Madinat El Bahr ni hatua kubwa ya mafanikio katika mipango ya maendeleo kwenye sekta ya utalii ambayo inachangia asilimia 27 ya pato la taifa na asilimia 80 ya fedha za kigeni.


Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa hoteli ya Madinat El Bahr iliopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar, hafla ambayo imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama na serikali pamoja na wawekezaji na wafanya biashara kadhaa kutoka katika sekta ya utalii.

Katika hotuba yake Rais Dk. Shein alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania, sekta ya utalii inachangia asilimia 80 ya fedha za kigeni zinazoingia Zanzibar ambapo taarifa za Kamisheni ya Utalii ya Zanzibar zinaeleza kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, utalii umechangia kiasi kikubwa katika upatikanaji wa ajira.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa ufanisi wa mipango na sera katika kuendeleza utalii unadhihirika wazi wazi katika matokeo ya utafiti juu ya sekta ya utalii uliofanywa na UNICEF kwa kushirikiana na Kamisheni ya Utalii Zanzibar mwaka 2018.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa idadi ya watalii wa kimataifa waliofika Zanzibar tangu mwaka 2008 hadi mwaka huu imekuwa ikiongezeka kwa kiwango kizuri ambapo hadi mwaka 1985 idadi ya watalii waliofika Zanzibar ilikuwa chini ya 20,000 ambapo hadi Disemba mwaka 2018 idadi ya watalii ilifikia 520,809.

Rais Dk. Shein alisema kuwa hayo ni matunda ya juhudi zilizochukuliwa ambayo yametokana na mipango bora na Sera sahihi ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mikakati mbali mbali, mpango wa Utalii kwa Wote na kuimarisha utawala bora ambayo inahakikisha mazingira ya amani, utulivu na usalama kwa wageni na wawekezaji.

Hata hivyo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuongezwa kwa  kasi na mipango bora zaidi katika kuwatembeza watalii kwenye makumbusho.