Maandamano katika uwanja wa ndege wa Hong Kong yaanza rasmi

Wanaharakati wanaodai demokrasia wameanzisha maandamano mengine ya siku tatu hii leo Ijumaa, katika uwanja wa ndege wa Hong Kong, wakitarajia kupata uungwaji mkono wa Kimataifa kwa abiria wanaowasili kupitia uwanja huo wa ndege, wakati maandamano yaliyoukumba mji wa Hong Kong yakiingia mwezi wake wa tatu.

Maandamano hayo yaliyohimizwa kupitia mitandao ya kijamii na kuwekwa karatasi za ruhusa ya kuingia katika ndege zenye maandishi ya mzaha "Uhuru wa Hong Kong" yatakuwa ya pili ambapo waandamanaji wameleta ujumbe wao katika kitovu cha safari za kimataifa.

Maandamano hayo ya leo yatakayodumu siku tatu hayajaidhinishwa rasmi lakini maandamano ya mwisho kama hayo katika uwanja huo, yalifanyika kwa amani bila ya usumbufu wowote wa safari za ndege.

Maandamano ya kupinga mswada uliyo na utata uliyotaka wahalifu wapelekwe China bara kufunguliwa mashtaka, yaligeuka na kuwa vuguvugu kubwa linalotaka uhuru zaidi mjini humo.