Mabilioni kujenga na kukarabati chuo cha Ufundi


Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa zaidi ya shilingi bilioni 4.6 kutekeleza mradi wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya majengo ya Chuo cha Ufundi cha Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe.

Hayo yamesemwa Wilayani Karagwe na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha katika ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya sekta ya elimu katika wilaya hiyo, ambapo amesema lengo la kutekeleza mradi huo ni kuongeza udahili wa wanafunzi wanaochukua masomo ya ufundi.

Ole Nasha amesema serikali imeweka mkakati wa kukarabati na kujenga vyuo vya ufundi katika kila wilaya, kwani ili kufikia uchumi wa viwanda ni muhimu kama nchi kuwa na vijana wenye maarifa na stadi mbalimbali za ufundi zitakazowawezesha kuajiriwa, kujiajiri na kushiriki katika uchumi wa viwanda.

“Rais ameweka nguvu nyingi katika kuinua uchumi wa nchi yetu, mnaona sasa miradi mikubwa inakuja, hospitali zinajengwa, barabara za lami nyingi zinajengwa, kwa hiyo kuna mambo mengi yanafanyika katika ujenzi na miradi yote hii yote yanahitaji ufundi, hivyo mtambue ufundi ni kitu muhimu sasa” ameongeza Ole Nasha.

Wakati huo huo, Naibu Waziri ametoa miezi mitatu kwa wakala wa majengo Tanzania (TBA) kuhakikisha wanamaliza ujenzi na ukarabati wa chuo hicho, ambapo amesema hajaridhishwa na sababu zilizotolewa na mhandisi msanifu kutoka TBA zilizopelekea kutokamilika kwa mradi kwa wakati.

Ole Nasha anesisitiza kuwa hakuna wakati wowote ambao fedha iliyopaswa kutolewa imeshindwa kutolewa na VETA kwani mpaka sasa TBA imeshalipwa zaidi ya shilingi bilioni moja ambayo ni asilimia 25 ya fedha yote iliyopaswa kulipwa wakati ujenzi umefikia asilimia 44 tu.

Awali Mhandisi Msanifu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Kelvin Joas alimweleza Naibu Waziri kuwa kutokukamilika kwa mradi huo kwa wakati nikutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo za kimkataba na kuwapelekea kuomba kuongezewa muda wa miezi sita baada ya muda wa mkataba kuisha Julai 26,2019.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Godwin Kitonka amesema Halmashauri yake inaishukuru serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kutenga fedha zaidi ya bilioni 4.6 kwa ajili ya kujenga majengo mapya ambayo ni pamoja na jengo la utawala, ukumbi mdogo, vyoo vya nje, bweni la wasichana na kukarabati karakana ya ushonaji na uchomeleaji chuma.

Mwanafunzi Masau Josephat, ameishukuru serikali kwa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia pamoja na kuongeza majengo ambayo awali hayakuwepo kwani mwanzoni hayakuwa yakiidhisha, huku wakiiomba serikali kuongeza baadhi ya kozi ambazo hazipatikani chuoni hapo ili kupanua wigo wa upatikanaji wa maarifa na stadi kwa vijana wa Karagwe na maeneo ya jirani.