Majaribio ya chanjo ya Ebola yaanza nchini Uganda

Watafiti nchini Uganda wamezindua majaribio makubwa zaidi ya chanjo ya úgonjwa wa Ebola ambayo inatarajiwa kupelekwa katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo iliyokumbwa na maradhi hayo hatari.

Majaribio hayo ya chanjo kutoka kampuni ya madawa ya Janssen yatajumuisha zaidi ya watu 800 na yanaungwa mkono na shirika la madaktari wasio na mipaka pamoja na shule ya afya na magonjwa ya kitropiki ya mjini London.

Pontiano Kaleeb ambaye anaongeza majarabio hayo amesema anasikitika kwamba chanjo ya Janssen haijafikishwa hadi sasa nchini DRC ambapo zaidi ya watu 1,800 wamekufa tangu maradhi ya Ebola yalipozuka mwaka uliopita.

Katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kuzuka kwa ugonjwa huo, zaidi ya watu 180,000 wamepatiwa chanjo ya majaribio ya Merck ambayo imeonesha mafanikio lakini waatalamu wana wasiwasi kuhusu upatikanaji wa chanjo hiyo wakati virusi vya Ebola vikisambaa hivi sasa kwenye mji wa Goma.