Watumishi wa umma waandamana Hong Kong

Maelfu ya wafanyakazi wa umma mjini Hong Kong leo wamekusanyika kuwaunga mkono waandamanaji na kutoa wito wa kurejeshwa kwa imani ya serikali wakati maandamano yakiendelea kuutikisa mji huo muhimu wa kibiashara barani Asia.

Mkusanyiko wa leo ni wa kwanza kufanywa na wafanyakazi wa umma kuonesha mshikamano kwa maandamano yaliyochochewa na muswada tata wa sheria ambao ungewezesha watuhumiwa wa uhalifu kupelekwa China Bara.

Watumishi hao wa umma walikusanyika kwa amani katikati ya kitovu cha mji wa Hong Kong wakiwa wameficha nyuso zao kuzuia kutambuliwa.

Maandamano zaidi yanapangwa kote mjini Hong Kong mwishoni mwa juma pamoja na mgomo uliondaliwa siku ya Jumatatu katika sekta muhimu ikiwemo uchukuzi ambao unatarajiwa kutatiza shughuli za kawaida kwenye mji huo.