Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), kuhakikisha inaandaa taarifa na kuambatanisha mkataba wa makubaliano kati yake na Kampuni ya Airport Development (KADCO) kuhusu uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kimanjaro (KIA) baada ya kugundua kuwapo taarifa zinazopingana.
Aidha, serikali imebainisha kuwa kupunguzwa kwa safari za ndege kulikofanywa na kampuni kubwa, kumechangia kushuka kwa mapato, yatokanayo na ada ya kutua na maegesho ya ndege.
Alisisitiza kuwa hali hiyo ni ya muda. Maagizo hayo yalitolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Naghenjwa Kaboyoka baada ya kupokea taarifa zinazopingana, moja ikionesha uwanja huo unamilikiwa na serikali kwa asilimia 100 na nyingine ikionesha KADCO inaombwa kutoa gawio kwa TAA kutokana na uendeshaji wa uwanja huo.
Alisema taarifa hiyo, ambayo inatakiwa kuonesha historia ya makubaliano ikiambatanishwa na nyaraka za Mkataba wa Makubaliano, inatakiwa kupelekwa kuhakikiwa na CAG na baadaye kufikishwa kwa Katibu wa Bunge ifikapo Novemba 1, mwaka huu.
Kaboyoka pia aliiagiza TAA kuhakikisha inajibu hoja za CAG na kuzipeleka ofisi ya CAG kwa ajili ya uhakiki na kuzifikisha kwa Katibu wa Bunge Novemba 1, mwaka huu.
Kamati imesikitishwa na TAA haina wataalamu wa kutosha na pia hoja za hesabu kutojibiwa ipasavyo jambo ambalo linaonesha hesabu hizi ni za kupikwa," alisema.
Kaboyoka pia aliiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, kufuatilia ripoti ya ukaguzi maalumu ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Songwe uliofanywa na CAG, na kujibu hoja zilizoibuliwa na taarifa ya majibu hayo kufikishwa kwa Katibu wa Bunge kabla ya Novemba 1, mwaka huu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Uchukuzi, Dk Leonard Chamuriho aliwaambia wajumbe wa PAC kuwa kampuni kubwa za ndege za Qatar na Emirates na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA), wamepunguza safari zao kutoka mbili kwa siku hadi moja.
"Ni bahati mbaya kwamba Shirika la Ndege la Etihad lenyewe limeamua kufuta kabisa safari zake hapa nchini," aliiambia kamati wakati wa kujibu hoja za wabunge walionesha wasiwasi wao wa kupungua kwa mapato kwa zaidi ya Sh bilioni 2.68 kulingana na taarifa ya CAG katika mwaka wa fedha wa 2017/2018.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TAA, Julius Ndyamukama aliiambia kamati hiyo kuwa tayari wameshaingia mkataba mpya na Kampuni ya Paytake and MPK Technology Limited kwa ajili ya kuboresha mfumo wa maegesho wa magari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Terminal I na II.