Mashine inayotumika kupima magonjwa ya ndani na kutambua taarifa katika mwili wa binadamu (ultrasound), imeibwa katika mazingira ya kutatanisha Hospitali ya Mji wa Bariadi ya Somanda mkoani Simiyu.
Inadaiwa kuibwa na kifaa chake cha kudurufu picha (printer).
Mashine hiyo ambayo ilikuwa maalumu kwa matumizi ya wodi mpya ya wajawazito na iliibwa ikiwa katika wodi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Mike Mabimbi, alisema mashine hiyo iliibwa Agosti 5 mchana, mwaka huu na hadi sasa haijapatikana.
Mabimbi alisema baada ya kutokea tukio hilo, walitoa taarifa polisi na watu 17 wakiwamo wauguzi walikamatwa kwa mahojiano.
“Ni kweli mashine hiyo ambayo ilitolewa na UNFPA kwa ajili ya wodi ya kina mama iliibwa katika mazingira ya kutatinisha, tayari taarifa tulitoa polisi na wanaendelea na uchunguzi,” alisema Mabimbi.
Alisema mashine hiyo inafanana kama kompyuta mpakato (potable), hivyo mtu yeyote mwenye nia ovu alikuwa na uwezo wa kuiba na kuweka katika begi la mgongoni na kutoweka nayo.
“Mashine hiyo ilitolewa kwa ajili ya kina mama wajawazito tu na ilikuwa humo humo kwenye wodi kwa ajili ya kurahisisha huduma, na wodi hiyo ilikuwa na vifaa vyote vinavyohitajika kwa mama mjamzito kikiwemo chumba cha upasuaji,” alisema Mabimbi.
Alisema baada ya kuibwa kwa kifaa hicho, wanalazimika kuwapeleka kina mama wajawazito katika mashine kama hiyo kubwa iliyoko chumba cha mionzi, takribani mita 10 kutoka wodi yao na kueleza kuwa inasababisha usumbufu.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Mwanaidi Churu, alisema mazingira ya kuibwa kwa kifaa hicho yameendelea kuwa magumu kutokana na watoa huduma katika wodi hiyo waliokuwepo siku hiyo kila mmoja kudai hajui.
