Matukio 910 ya ukatili na udhalilishaji wa Kijinsia yaripotiwa kutokea


Na Thabit Madai, Zanzibar

Jumla ya matukio 910 ya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia  kwa wanawake na watoto Zanzibar yameripotiwa kutokea kwa kipindi cha mwaka Mmoja  kuanzia Januari Mosi 2018 hadi Disemba 31, 2018.


Matukio hayo ni Ubakaji,Kulawiti, kuingilia kinyume na maumbile, kutorosha , Shambulio la aibu pamoja na shambulio la kawaida.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Idara ya Takwimu za Kijamii na Demografia kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali,Khadija khamis Hamadi wakati akiwasilisha  Takwimu za vitendo vya ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto Zanzibar kwa mwaka 2018 katika Ofisi za Wizara ya Kazi, Wanawake , Wazee na Watoto Zanzibar.

Mkuu huyo wa Idara ya Takwimu alisema kuwa kwa kipindi cha mwaka wa 2018 matukio yaliyoripotiwa kutokea ni 910 kwa wilaya zote 11 unguja na Pemba.

Alisema katika matukio hayo matukio ambayo yanaongoza kuripotiwa kwa wingi ni matukio ya ubakaji kwa watoto  huku wilaya ya Magharib B Unguja ikiongoza kwa matukio 112 na ikifuatiwa na wilaya ya Mjini Unguja matukio 79 kwa mwaka huo.

“Mbali na Matukio hayo matukio mengine ambayo nayo yameripotiwa kwa wingi kwa mwaka huo kama vile  kulawiti na kuingilia kinyume na maumbile ambapo kwa yote  Idadi yake ni 107” alieleza Mkuu huyo wa Idara ya Takwimu za kijamii na demegrafia khadija khamis Hamadi.

Aidha alieleza kuwa kwa kesi za kutorosha, Shambulio la aibu na Shambulio la kawaida kwa mwaka 2018 kesi zilizoripotiwa jumla yake ni 224 kwa wilaya zote unguja na Pemba.

Alifafanua kuwa katika uwiano wa asilimia kwa namana matukio yalivyoripotiwa wilaya ya Magharib B inaongoza kwa kesi zote sawa na asilimia 13.2 ikifuatiwa na wilaya ya Chake chake Pemba  asilimia 12.7 , Wilaya Magharib A Unguja asilimia 12.2 na wilaya ya Wete Pemba Asilimia 12.0.

“Na Wilaya nyingine ambazo zinafuata kwa uwiano huo huo wa asilimia ni Wilaya ya Mjini Unguja asilimia 9.5, Kaskazin A 9.0, Kaskazini B 8.7, Mkoani Pemba 6.4, Kusini Unguja 4.7 na wilaya ya Micheweni 2.9 kati ya kesi zote zilizoripotiwa.

 Mapema Akizungumza Naibu katibu Mkuu Wizara ya kazi Uwezeshaji Wazee, Wanawake na Watoto Mwajuma Majid Abdalla alisema kuwa Zanzibar ni moja sehemu ambayo inakumbw na janga la vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto kwa kiasi kikubwa hali hiyo inapoteza mueleko wa taifa.

“Katika kupambana na vitendo hivyo tumebaini kuwa vitendo hivi vinasababishwa kutokana na kuwepo kwa Mmong’onyoko wa maadili katika jamii zetu”alibainisha Naibu Katibu Mkuu huyo.

 Aidha alieleza kuwa katika vkukabiliana na vitendo hivyo Wizara imeamua kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu wa Serikali katika kukusanya takwimu sahihi za vitendo hivyo ili kuwapatia wadau na kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya vitendo hivyo.

“Katika kulifanikisha suala hili kama wizara tumeona ni vyema kushirikiana Na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali imechukua juhudi za kutosha za kuhakikisha uimarishaji wa upatikanaji wa takwimu halisi za ya tatizo hili”alibainisha Mkuu naibu huyo Mwajuma Majid.

Nae Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mayasa Mahfoudhi Mwinyi alisema kuwa kutoka na kushamiri kwa vitendo hivyo na uwepo wa Takwimu zisizo sahihi kwa wadau wa kupambana na vitendo hivyo ndo maana taasisi hizo mbili zimekubalina kutoa kufuatilia na kuzitoa kwa pamoja ambazo zitakuwa sahihi.

“Kwa sasa tumeamua kufuatilia na kuzitoa takwimu hizo kwa wadau ili wabaini ukumba wa tatizo na kuanza kupambana nalo kwa nguvu zote” alisema Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mayasa Mahfoudhi Mwinyi.

Aidha alisema Mpango huo wa kuzitoa Takwimu hizo utakuwa endelevu ambapo kila robo tatu ya mwaka zitakuwa zinatolewa kwa dau na kuzidi kuongeza kasi na mapambano dhidi ya vitendo hivyo.
Mpya zaidi Nzee zaidi