Meli ya mafuta ya Iran huenda ikaachiwa

Meli ya mafuta ya Iran iliyokuwa ikishikiliwa Gibraltar kwa kukiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya huenda ikaruhusiwa kuondoka hii leo ingawa jitihada za mwisho mwisho za kisheria za Marekani kutaka kuizuia meli hiyo kuondoka huenda zikaishia mahakamani.

Waziri Kiongozi wa Gibraltar Fabian Picardo amesema Gibraltar imeamua kuiachia meli hiyo lakini haikueleza mara moja ni wakati gani ama iwapo meli hiyo itaanza safari baada ya Marekani kuanzisha mchakato wa jaribio la kisheria la kuizuia.

Picardo alikiambia kituo cha redio cha shirika la habari la Uingereza, BBC kwamba meli hiyo inaweza kuondoka mara baada ya kukamilisha utaratibu wote muhimu wa kuendelea na safari yake. Aliongeza kuwa inaweza kuwa tayari kuondoka leo ama kesho.