Miradi sita ya Shilingi Bilioni 8.7 yawekwa mawe ya msingi Wilayani Bahi



Na.Enock Magali Dodoma

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa kwa mwaka 2019 Mzee Mkongea Ally amezindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi 6 katika Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Mkoani Dodoma yenye thamani ya sh bil 8.7 huku akiwataka viongozi na wananchi kuilinda miradi hiyo ili idumu.

Baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa maboma manne katika shule ya sekondari ya Mundemu uliowekwa jiwe la msingi,mradi wa usambazaji maji kijiji cha Mkakatika uliogharimu zaidi ya mil 600 na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya km 2.3 katika mji wa Bahi ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyowahi kuitoa Mh.Rais Dkt John Pombe Magufuli wakati wa kampeni mwaka 2015.


Akizungumza Agost 18 mara baada ya kukagua miradi hiyo Mkongea amesema Rais Dkt John Magufuli anatumia fedha nyingi kupeleka kwenye miradi ili iwasaidie wananchi hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuilinda.

"Katika mradi huu wa maji wa Mkakatika tumetumia muda mrefu kujiridhisha ili tuone thamani ya fedha, na baada ya ukaguzi huo tumeridhishwa na natamka kwamba Mwenge wa Uhuru 2019 umeridhia kuweka jiwe la msingi mradi huu,"alisema Mkongea.

Pamoja na kuridhia kuweka jiwe la msingi alitoa maelekezo ikiwemo kuhakikisha mkandarasi wa ujenzi anapeleka vipimo katika maabara ya serikali.

"Mradi huu nimeambiwa bado haujakamilika, hivyo nisisitize mambo mawili, moja kuhakikisha fedha zilizobaki zinatumika kukamilisha mradi huu, pili mkandarasi ahakikishe anapitisha vipimo vyote katika maabara ya serikali,"aliongezea Mkongea.

Akikagua ujenzi wa hospitali ya wilaya Mkongea aliwapongeza na kusema ujenzi huo umetekelezwa vizuri na thamani ya fedha imeonekana.

Alisema ametembelea ujenzi wa hospitali nyingi zilizopewa sh bil 1.5 lakini nyingine bado ndio wanapaua na kusema kuwa Bahi ni hospitali ya kwanza kati ya zote alizotembelea.


Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Bahi Mwanahamisi Munkunda aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano waliouonyesha wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.

"Mafanikio tunayoyapata yanatokana na ushirikiano wa wananchi na ushirikiano uliopo baina yetu sisi watumishi, tukuahidi kufanyia kazi maelekezo yote,"alisema Mkuu wa wilaya huyo

Mwenge wa Uhuru pia ulitembelea mradi wa utunzaji wa chanzo cha maji na uhifadhi wa msitu wa Chenene uliopo kijiji cha Mayamaya, uliweka jiwe la msingi mradi wa kuzalisha kokoto katika kiwanda cha kokoto cha kampuni ya KASCCO.