Mke na mume watupwa Jela miaka 5 kwa kuwakeketa watoto wao watatu


Watu wawili ambao ni wanandoa wamewahukumu kifungo cha miaka mitano jela na Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, kwa kosa la kuwakeketa watoto wao watatu. Wazazi hao ni
 Thadei Parokwa (43) na mke wake Lowema Thadei (34),

Mwendesha mashitaka wa Polisi mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Mkaguzi wa Polisi, Hamilton Moses, amesoma shitaka lililowakabili washitakiwa hao kuwa ni ukatili dhidi ya watoto.

Amesema kesi hiyo iliripotiwa kituo cha Polisi Orkesmet tarehe Machi 19, mwaka jana baada ya kukamatwa watuhumiwa hao ambao walidaiwa kuwakeketa watoto hao kwa bibi yao aliyekuwa Kitongoji cha Kangala Kijiji cha Lobosireti Wilayani humo.

Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Lugano Kasebele, baada ya kujiridhisha kwa pande hizo mbili, aliwatia hatiani wazazi hao kwenda jela miaka mitano ama faini ya laki sita na fidia ya laki tisa.

Alisema vitendo vya ukeketaji vimekuwa vikifanyika kwa kificho wilayani humo, pamoja na uwepo kwa sheria bado vinaendelea kujitokeza hivyo wanatakiwa kutumikia adhabu hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hizo.

Kwa upande wake Miltone, alimwomba Hakimu wa mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa wahusika kwani vitendo hivi vimekithiri wilayani humo huku madhara yakiendelea kujitokeza.