Polisi Hong Kong wafyatua mabomu ya kutoa machozi kuwakabili waandamanaji

Polisi wa Hong Kong wa kukabiliana na ghasia wamefyatua mabomu ya kutoa machozi na kutumia virungu kuwakabili waandamanaji waliojibu kwa kuwarushia mawe, chupa na fimbo za mianzi, wakati makabiliano yao katika mtaa mmoja wa mji huo yalipogeuka kuwa machafuko, na kuvunja hali ya amani iliyokuwepo kwa siku kadhaa zilizopita.

Awali, maelfu ya waandamanaji, wengi wao wakiwa wamevalia kofia za kuzuia gesi kuingia puani na machoni, waliandamana katika eneo la kiviwanda la Kwun Tong, ambako walizuiwa na kikosi cha polisi wa kukabiliana na ghasia wakiwa na ngao na virungu nje ya kituo cha polisi.

Maandamano ya Hong Kong yalizushwa na miito ya kuzuwia muswada ambao haupendelewi wa kuwapeleka wahalifu China bara.