Rais wa Iran aijibu Marekani

Rais wa Iran Hassan Rouhani leo ameituhumu Marekani kwa kile alichokiita "tabia ya kitoto" baada ya Marekani kumuwekea vikwazo Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif wakati ambapo kuna hali ya wasi wasi inayoongezeka kati ya nchi hizo mbili.

Rouhani amesema katika kauli iliyopeperushwa moja kwa moja katika televisheni ya kitaifa nchini Iran, kwamba Marekani "walikuwa wanasema kila siku wanataka yafanyike mazungumzo bila masharti yoyote, na sasa wanamuwekea vikwazo waziri wa mambo ya nje, hii ina maanisha kwamba wamepoteza uwezo ya kufikiria vyema." Ikumbukwe kwamba Marekani awali iliwahi kupendekeza mazungumzo yasiyokuwa na masharti na Iran.