Serikali yajipanga kuongeza ushirikiano Sekta binafsi


Serikali imesema kuwa imejipanga lkuongeza ushirikiano na Sekta binafsi  katika kuhakikisha kuwa kero na vikwazo vinaondolewa ili kuweka mazingira bora ya biashara na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ameyasema hayo leo wakati akimuwakilisha Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa kufungua Mkutano mkuu wa mwaka wa dharura wa TCCIA mwaka 2019 huku akiongeza kuwa serikali imefanya uamuzi mahususi mwaka huu wa kuondoa muingiliano wa utoaji wa huduma za  mashirika ya TBS na TFDA ili kupunguza usumbufu kwa Wanyabiashara.

Alisema kuwa hizo ni hatua za awali na ametoa mwito kwa TCCIA kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanafuata sheria, kanuni na taratibu zote zilizowekwa ili kuondoa usumbufu wote unaoweza kujitokeza wakati wa kufanya biashara.

Alisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli alizindua  Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Kilimo (ASDPII) tarehe 4 Juni, 2018. Kwa kutambua umuhimu wa Sekta Binafsi, moja ya maboresho makubwa ya ASDP II ukilinganisha na ASDP I ni kuipa nafasi kubwa zaidi Sekta Binafsi.

Aliongeza kuwa ni wakati muafaka wa kubaini maeneo maalumu ambayo Taasisi hiyo ya TCCIA itaendelea kutoa mchango mkubwa katika kutekeleza programu hiyo ili iweze kufikia malengo
yaliyowekwa.

Hasunga amesema kuwa ili kuhakikisha uboreshaji wa Mazingira ya biashara nchini, Serikali kwa
kushirikiana na Sekta Binafsi iliandaa andiko maalumu “Blue Print” ambalo lilikwisha zinduliwa, pia mpango wa utekelezaji wake umeandaliwa na umeanza kutekelezwa.

“Ni wajibu sasa wa kila pande yaani Sekta ya Umma na Binafsi kuhakikisha kuwa yale yote yaliyoainishwa katika andiko hilo yanatekelezwa ipasavyo,” Alikaririwa  Hasunga.

Vile vile, amesema kuwa serikali imeendelea na jitihada za kuimarisha Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Wilaya ambapo tayari imeshaweka Mwongozo wa Mabaraza hayo ambayo TCCIA ni Sekretarieti.

Waziri Hasunga amewataka washiriki hao kuchangamkia  fursa zilizopo katika miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali nchini, hasa miundo mbinu ya reli ya Kisasa, mradi wa umeme wa bwawa la Nyerere, barabara za kisasa, bomba la mafuta, manunuzi ya ndege n.k.

Alisema kuwa Fursa hizo kwa kupitia sera ya “Local Content” nao wakiwa wazawa wana nafasi kubwa ya kunufaika nazo.

Amesema, Miradi hiyo ni mingi na itachukua muda mrefu ikitekelezwa kwa awamu tofauti. “Endapo kwa sababu moja au nyingine haukuweza kupata fursa ya kushiriki kazi kwenye mradi mmoja kwa sababu fulani zikiwemo sifa kadhaa basi, nakushauri ujipange vizuri kwenye miradi inayokuja, msikate tamaa” Alisisitiza Hasunga.


Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia