Serikali yawaonya wanaoshabikia Ndege ya ATCL kuzuiwa


Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma

Serikali imewatahadharisha watanzania ambao wanahusika au kushabikia kitendo cha ndege ya Shirika la ndege hapa nchini kushikiriwa na mahakama ya Afrika kusini, kwani kufanya hivyo ni sawa na kesi ya uhujumu uchumi.

Pia amebainisha kuwa ndege hiyo inashikiliwa kwa agizo la mahakama lakini Serikali ya Tanzania tayari imewasilisha hoja tatu nzito, juu ya tukio hilo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo (Agosti 31, 2019) Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa Serikali kwa mwezi Agosti 2019.

Dkt. Abas anasema kwa Sasa serikali hauwezi kusema chochote kwa sababu kesi ipo mahakamani, lakini tu ujumbe uwafikie wale wanaojihusisha na vitendo hivyo ni sawa na kesi ya uhujumu uchumi.

"Tunasubir majibu ya mahakama na tumewasilisha hoja nzito na watetezi upande wa pili wameanza kutetemeka, ujumbe kwa Hawa Sasa watanzania wenzetu wanaotuhujumu wajue tunasubir kesi iishe tutawashughulikia" amesema Dkt Abas.

Amesema kwa ujumla serikali haitakubali kuyumbishwa, na inaendelea na kuchapa kazi kuwatumikia watanzania, na haitarudi nyuma katika mapambano.

Aidha, Dkt Abbasi ameabainisha kuwa jumla ya shilingi bilioni 25.5 zimerejeshwa Serikalini kwa mchanganuo ufuatao; bilioni 14.6 ikiwa ni urejeshwaji wa mali zilizopatikana kwa njia ya uhalifu na bilioni 10.9 zilizotokana na thamani ya mali zilizotaifishwa yakiwemo magari, vituo vya mafuta, nyumba nane, magari nane na  Bilioni 20 ambazo ni mali zilizozuiwa kesi zikiendelea.

Amesema kuwa kwa upande wa Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imeokoa takribani shilingi bilioni 46.9 zilizokuwa zipotee kutokana na kutofuatwa taratibu za ununuzi, malipo ya zaidi ya mkataba kwa wakandarasi au baadhi kutorudisha fedha walizopewa kama dhamana na uzembe na rushwa.

Akizungumzia utekelezaji katika sekta ya uchukuzi, Dkt. Abbasi amesema kuwa Serikali imeanza zabuni ya kuagiza vichwa 22 (vitano vya mafuta yaani Diesel Locomotive na 17 vya umeme yaani Electrical Locomotive) na mabehewa ya abiria 60 na 1430 ya mizigo.

Aidha ameongeza kuwa, Serikali imeanza zabuni ya treni tano (5) zilizokamilika (Electrical Multiple Unit) za abiria zenye mabehewa nane (8) kila moja na vichwa viwili kwa ajili ya uendeshaji wa treni za abiria kwa kipande cha Dar es salaam hadi Morogoro na kisha Dodoma.

Mbali na hayo, ameeleza kuwa, Serikali imetenga fedha za ndani shilingi Bilioni 71.4 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja jipya la Mto Wami lenye urefu wa Mita 513.5 litakalojumuisha ujenzi wa barabara za KM 4.3 kwa kila upande ambapo kazi ya ujenzi huo imeshaanza.

Pia, Serikali imesaini mkataba wa shilingi bilioni 699.9 kwa ajili ya ujenzi wa Daraja refu zaidi Afrika Mashariki na Kati la Kilometa 3.2 kuunganisha mikoa ya Mwanza na Geita kwenye eneo la Kigongo-Busisi katika Ziwa Victoria.

“Niwathibitishie Watanzania kuwa azma yetu ya kuiendeleza nchi kwa kasi chini ya Jemedari Dkt. John Pombe Magufuli inaendelea kushika kasi na katika hili hakuna mwanadamu wa  kutuzuia wala kuturudisha nyuma” amesema Dkt Abbasi.