Wafanyabiashara Makambako wailalamikia TARURA



Na Amiri kilagalila-Njombe

Wakala wa barabara vijijini na mijini (TARURA) halmashauri ya mji wa makambako mkoani Njombe umelalamikiwa na wafanyabiashara kwa kitendo cha kuzuia baadhi ya magari yenye zaidi ya tani kumi yasiingie kwenye maeneo muhimu husasani kwenye masoko ya mbao pamoja na magodauni ya kuhifadhia mazao na bidhaa zao.

Wakizungumza na MUUNGWANA BLOG  baadhi ya wafanyabiashara wamesema kuwa kitendo ambacho kimefanywa na Tarura kimewaathiri kwa kiasi kikubwa kwa kuwa wameshindwa kusafirisha bidhaa na mazao yao kutokana na barabara zinazo fika katika maeneo hayo muhimu kuzuliwa .

“Unapo mkamata huyu mwenye magari utakuta mfanyabiashara anasubiri zaidi ya masaa matano inamaana tayari tunaathiri uchumi wetu wenyewe,lakini pia hatujua halmashauri inataka tupeleke vipi bidhaa kwenye magodauni”walisema baadhi ya wafanyabiashara

Mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara mkoani Njombe Siphael Msigala ameitaka serikali kutumia hekima katika utekelezaji wa sheria zilizopo ili waweze kufikia lengo walilojiwekea badala ya kutumia amri pekee ambayo inawaathiri wafanyabiashara.

“Mji wetu wa makambako ni mji wa kibiashara lazima watendaji wote wanaokuja wakafahamu,hivyo unapokuja kutimiza sheria Fulani ni vizuri ukajipanga vizuri vinginevyo unaweza kuleta machafuko yasiyokuwa ya lazima,unapoziba barabara ambazo hata wakati mwingine greda halijawahi kusafisha unafungashaje sasa bara bara kama hiyo iliyokuwa inatumika wakati wote”alisema Msigala

Kwa upande wake meneja wa tarura halmashauri ya mji wa makambako Mhandisi Anyetike Kasongo amesema wamezuia magari yenye uzito zaidi ya tani kumi yasipite katika barabara hizo kutokana na kutengwa kwa ajili ya magari yenye tani chini ya kumi na kueleeza kuwa licha ya zuio hilo lakini wamewaruhusu wafanyabiashara waendelee kutumia baadhi ya barabara  hususani zile za mhimu zaidi katika kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.

“Kweli tumeweka vibao wasizitumie hizo barabara wakati tunaangalia namna nyingine ya kuweza kurekebisha ili ziweze kubeba uzito huo,kwa bahati mbaya kuna maeneo ambayo yamejengwa magodauni basi tumekubaliana bara bara za vumbi watumie kwa muda wakati tunaangalia maeneo yaliyotengwa na halmashauri kwa ajili ya kuingiza na kutoa mizigo yao”alisema Anyetike kasonga