Wakazi 650 wasahau shida ya Maji


Wakazi 650 wa Kijiji cha Sangara wilayani Babati mkoa wa  Manyara, wameondokana na changamoto ya muda mrefu wa ukosefu wa maji.

Wameachana na usumbufu huo , baada ya mradi wa maji uliogharimu  Sh. milioni 229 kuzinduliwa.

Mradi huo unatoa lita 352,800 kwa siku, sawa na lita 14,700 kwa saa, unahudumia watu kwa utaratibu wa kulipia huduma  kabla ya kuipata yanayofanyika kwa njia ya kielektroniki.

Mkurugenzi wa shirika la kimataifa la  Water Aid, Abel Dugange, akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi huo alisema, waliingia makubaliano ya kutekeleza mradi huo mwaka jana na halmashauri ya Wilaya ya Babati, Shirika la Habitat for Humanity, kampuni ya eWater na taasisi ya fedha ya Unit Trust of Tanzania (UTT-MFI).

Dugange alisema kabla ya kutekeleza mradi huo upatikanaji wa maji kwenye kijiji hicho, ulikuwa asilimia 20 tofauti na lengo la taifa la asilimia 85 ya huduma za maji vijijini.

"Mradi huu umelenga kuhamasisha ubunifu na kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu na uendeshaji wa miradi ya maji ili kurahisisha upatikanaji wa huduma endelevu na hakika ya maji safi na salama vijijini," alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Elizabeth Kitundu akizindua mradi huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti, aliwataka wakazi wa eneo hilo kuutunza ili uwe endelevu.

Kitundu alisema lengo la serikali ifikapo mwaka 2020 ni kuona kuwa asilimia 85 ya watu waliopo vijijini wanapata maji safi na salama na mwaka 2025 iwe asilimia 95 na mwaka 2030 iwe asilimia 100.

Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Vrajilal Jituson, alisema mradi huo ni wa mfano kwani umeanzia Babati kisha Wilaya za Korogwe mkoani Tanga na Arumeru mkoani Arusha zikafuata.