Wananchi wamtaka Mbunge wao kutatua shida ya maji


Wakazi wa Kata ya Misasi, Wilayani Misungwi, Mkoa wa Mwanza wamemuomba Mbunge wao, Charles Kitwanga, awasaidie kutatua shida ya upatikanaji maji katika kata yao.

Wakizungumza wakati wa mkutano wa Mbunge huyo uliofanyika katika viwanja vya CCM Misasi, mmoja wa wakazi wa kata hiyo, Charles Chome, alisema tatizo la maji limekuwa likiwasumbua kwa muda mrefu na kuharibika kwa mashine ya kijiji ya kusukuma maji kumeongeza kero hiyo kuwa kubwa zaidi.

Alisema shida hiyo imekuwa changamoto kwao jambo linalosababisha wake zao kurudi majumbani usiku kutokana na kushinda kwenye foleni ya kusubiri kuchota maji.

Meneja Usambazaji Maji Vijijini Wilayani Misungwi, Mafasila Maduka, alisema kero ya maji ni tatizo kubwa kwao, lakini wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha mradi mkubwa wa maji katika Kata ya Misasi.

Alisema mpaka sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 50 na wapo katika hatua nzuri ya uwekaji mabomba. Aliahidi kuwa mradi huo wa maji utakamilika Novemba mwaka huu na kwamba zaidi ya wananchi 59,000 watanufaika.

Kwa upande wake, Kitwanga alisema mradi huo wa maji wa Misasi umegharimu Sh bilioni 12 na vijiji 17 vitafaidika nao. Alivitaja baadhi ya vijiji kuwa ni Nyangomango, Igelele, Mbalika, Ngaya, Matare na Misasi.
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia