Bibi ahukumiwa miaka 99 jela


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu kifungo cha miaka 99 jela, Bibi Salma Mntambo baada ya kupatikana na hatia katika mashitaka 17 ikiwemo kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Miaka hiyo 99 inatokana na makosa 14 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ambapo kwa kila kosa amehukumiwa miaka sita jela, huku katika makosa matatu ya kutoa nyaraka za uongo kila kosa akihukumiwa miaka mitano jela.

Hata hivyo mshitakiwa huyo atatumikia kifungo cha miaka 6 jela kwa sababu miaka hiyo itaenda sambamba.

Hukumu hiyo, imetolewa na Hakimu Mfawidhi, Kelvin Mhina ambapo amesema amepitia sababu za upande wa mashtaka na utetezi katika kesi hiyo, hivyo katika makosa matatu ya kutoa nyaraka za uongo mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka mitano jela kwa kila kosa.

Pia katika makosa 14 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka sita jela kwa kila kosa.

"Huo ndio uamuzi wa mahakama lakini mna haki ya kukata rufaa, kuhusu suala la fidia nitatafakari na kufanya utafiti ili nije kutoa oda ambayo ni sahihi hivyo Oktoba 2, mwaka huu nitaitoa oda hiyo ya fidia” amesema Hakimu Mhina

Mshtakiwa huyo alikuwa akikabiliwa na mashtaka 24 na ametiwa hatiani katika mashtaka 17 yakiwamo ya kutakatisha fedha jumla ya Tsh. Bilioni 1.027,000,000 kutoka kwa Ridhuan Mringo huku akijua fedha hizo zimetokana na zao la makosa tangulizi ya kugushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuwasilisha nyaraka za uongo.

Katika kosa la kugushi, mshtakiwa Mntambo anadaiwa kati ya June mosi 2003 na Oktoba 31, 2011 maeneo yasiyojulikana Wilayani Ilala, Mkoani DSM kwa nia ya udanganyifu aligushi risiti yenye namba 001226 ya tarehe 10/06/2003 ili kuonesha kwamba Ridhuan Mringo alinunua nyumba ya Shirika la nyumba iliyopo Plot namba 710 mtaa wa Mfaume Upanga kwa Tsh. Millioni 70 wakati akijua ni uongo.