Bugando yaokoa Mabilioni kwa matibabu ya Saratani


Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC) imefanikiwa kuokoa zaidi ya Shilingi bilioni mbili kwa wananchi wa kanda ya ziwa kusafiri kwenda jijini Dar es Salaam kupata matibabu ya saratani kila mwaka.


Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Prof. Abel Makubi wakati akiongea na Maofisa habari wa Wizara ya Afya na Taasisi zake waliokuwepo jijini Mwanza kwa ajili ya kujionea mafanikio ya utoaji huduma za afya kwa wananchi.

Prof. Makubi alisema kuwa kuanza kwa tiba ya saratani katika Hospitali ya Kanda Bugando imesaidia kuokoa kiwango cha fedha hizo kutoka kwa wananchi wa kanda ya ziwa ambapo awali iliwalazimu kusafiri hadi Jijini Dar es Salaam kupata huduma hizo kwenye Hospitali ya Saratani ya Ocean Road.

“Tunaishukuru Wizara ya Afya ambayo ilitupatia kiasi cha Shilingi bilioni 5.5 kwa ajili ya kujenga jengo la saratani. Kama hospitali tumeweza kununua mashine nne za mionzi na dawa kwa kushirikiana na wafadhili wengine”.

Aidha, alisema, hivi sasa asilimia 90 ya wagonjwa hawapelekwi wanapata huduma hapa hivyo kuwaondolea adha ya kusafiri na kupata huduma mbali wananchi wa kanda ya ziwa ambapo awali zaidi ya asilimia 50 ya wagonjwa wa saratani wa Ocean Road walikuwa wakitoka kanda hiyo.

Naye Mtaalam wa Tiba Mionzi wa Idara ya Saratani wa BMC, Alex Mpugi alisema kabla ya mashine hizo walikua wakitoa huduma za saratani kwa kutumia kemikali.

“Naomba nitoe wito kwa wananchi hususan wanawake kujitokeza kufanya uchunguzi wa saratani ya shingo ya uzazi na matiti kila siku ya Jumanne na Alhamis”.Alisisitiza Mpungi.

Kwa upande wa Upasuaji Mkurugenzi wa Upasuaji Dkt.Fabian Massaga alisema kuwa,Hospitali imefanikiwa kufanya ukarabati na upanuzi wa vyumba vya upasuaji kutoka vyumba sita hadi kumi na tatu ambapo vyumba viwili hutumika kwa upasuaji wa dharura na kimoja kwa ajili ya upasuaji kwa akina mama wajawazito.

Aliongeza kuwa kwa upande wa upasuaji wameweza kuongeza idadi ya wagonjwa kutoka ishirini na tano hadi hamsini na hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa wengi waliokuwa wanasubiri upasuaji kwa miezi mitatu lakini hivi sasa wanafanyiwa upasuaji ndani ya wiki moja.

Hata hivyo Dkt. Massaga alisema upanuzi huo umeendana na ununuzi wa vifaa vipya na vya kisasa ikiwemo vitanda vya kufanyia upasuaji, taa maalumu za vyumba vya upasuaji na mashine za kisasa kabisa za kutolea dawa ya usingizi. Vifaa hivi vimeagizwa moja kwa moja viwandani kwa takribani Shilingi bilioni 1.4 badala ya Shilingi bilioni 3 kama wangenunua kwa wauzaji hapa nchini.