Faida zitokanazo na matumizi sahihi ya mchaichai

Mchaichai ni mmea unaostawishwa katika maeneo mengi nchini. Mara nyingi majani yake yanachemshwa ili kupata kinywaji chenye harufu na ladha nzuri.

Ladha na harufu yake vinawavutia wengi kuinywa hata yule ambaye hakuwahi kuionja. Hata hivyo, kuna swali la kujiuliza je, wote wanaokunywa wanajua faida za kiafya wanazopata kutokana na chai ya mchaichai?

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali ni kwamba mchaichai una vichocheo muhimu vinavyoweza kupambana na athari mbalimbali za maradhi tumboni, kwenye njia ya mkojo na hata kwenye vidonda.

Mchaichai pia ni kinywaji ambacho kinasaidia kupunguza joto la mwili hususani kwa wenye dalili za homa.

Kinywaji hiki kinasaidia kurahisisha mmeng’enyo wa chakula tumboni, lakini pia kutoa nafuu kwa wenye matatizo ya magonjwa ya kuhara na maumivu ya tumbo ikiwamo tatizo la kujaa gesi. Mwathiriwa anywe chai yenye majani hayo pekee kwa siku tatu mfululizo asubuhi na jioni.

 Mchaichai pia unasaidia kuondoa hali ya kiungulia na kuzuia kutapika au kuhisi hali ya kichefuchefu mara kwa mara pamoja na kupunguza kiwango cha sumu za mwilini na hivyo kulinda afya ya figo.

Sanjari na hayo, kutumia majani ya mchaichai kunasaidia kuondoa maumivu ya mwili sehemu mbalimbali na kupunguza maudhi kwa kinamama wakati wa hedhi.

NAMNA YA KUTUMIA
 Chukua majani ya mchaichai kiasi, yaoshe vizuri na baadaye yachemshe. Baadaye maji yake mimina kwenye chupa ya chai tayari kwa kunywewa. Kunywa maji hayo kutwa mara mbili muda wa wiki moja hadi mbili mfululizo.