Nchi ya Kenya imeanza kufanya majaribio ya sehemu mpya ya reli ya kisasa, SGR ambayo inatoka katika jiji la Nairobi hadi Suswa kwenye eneo la Bonde la Ufa.
Ujenzi wa reli hiyo ambayo inatarajiwa kuimarisha usafirishaji wa bidhaa na abiria unatekelezwa na kampuni ya China (China Communications Construction Company).
Sehemu hiyo yenye umbali wa kilomita 120 ni awamu ya kwanza ya mradi huo wa reli ambayo hatimaye itafika katika mji wa Malaba kwenye mpaka wa Kenya na Uganda. Kenya tayari imekamilisha na inatumia awamu ya kwanza ya mradi huo wa SGR kutoka mji wa Mombasa hadi Nairobi, umbali wa kilomita 472.

