RC Ayoub apokea Boksi 750 za Mchele


Na Thabit Madai-Zanzibar

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib Unguja, Ayoub Mahamed  Mahmoud  ameziomba Taasisi zisizo za kiserikali, Wafanyabiashara na wadau mbali mbali wa maendeleo kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika kuinua Sekta ya elimu Nchini.

Wito huo ameutoa leo Septemba 15 wakati akipokea msaada wa mchele boksi 750 kwa niaba ya wakuu wa mikoa yote mitano Unguja na Pemba. Msaada huo wa Mchele umetolewa na Jumuiya ya kusaidia jamii Muzdalifa kwa wanafunzi wa kidato cha Nne.

Hafla hiyo ya kukabidhi mcheleo huo boksi 750 kwa skuli za Unguja na Pemba imefanyika katika ukumbi wa skuli ya Haile salas Mjini Unguja na kuhudhuriwa na wakuu wote wa Mikoa  ya  Zanzibar.

Ayoub alisema Taasisi zisizo za kiserikali, wafanyabiashara na wadau wa maendeleo hawana budi kusaidia jamii katika sekta ya elimu ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Dkt Ali Mohamed Shein.

"Kiukweli Serikali yetu ya mapinduzi inafanya kazi kubwa katika kuinua elimu nchini hivyo niwaombe taasisi nyingine zisiszo za kiserikali, wafanyabiashara kusaidia katika elimu ili tuwe na taifa la wasomi" alisema mkuu huyo wa Mkoa.