RC Dodoma azindua mkakati wa huduma ya Afya ya Uzazi wa Mama,Vijana na Mtoto



Na,Enock Magali,Dodoma.

Mkoa wa Dodoma umezindua mkakati wa huduma ya afya ya uzazi wa mama,vijana na mtoto ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizopo vifo vimeonekana kupungua kutoka 85 mwaka 2010 hadi vifo 67 mwaka 2018.

Aidha Mkakati huo ni wa miaka mitano utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 43.

Akitoa taarifa ya hali ya Afya ya mama na mtoto mkoani humo, Mratibu wa Huduma ya Afya ya uzazi, vijana, mama na mtoto Marry Shedrack ametaja sababu saba zinazochangia  vifo hivyo ikiwemo uzazi pingamizi na matumizi ya dawa za miti shamba.

Pia ametaja sababu nyingine zinazosababisha vifo hivyo kuwa ni kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua, kifafa cha mimba,upungufu wa damu,kuchanika kwa mfuko wa uzazi,uambukizo na matatizo ya dawa ya usingizi.

Amebainisha changamoto mbalimbali zinazosababisha vifo hivyo kuwa ni pamoja na umbali wa kufika kwenye vituo vya kutolea huduma na ukosefu wa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya uzazi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Options ambaye ni kiongozi wa timu ya mradi wa WISH Dokta Moke Magoma amesema kama wadau wa afya wamejipanga kuhakikisha mpango huo unatekelezeka na wapo tayari kutoa ushirikiano.

Akitoa maelezo kuhusu mpango huo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma dokta BEST MAGOMA amesema  mkakati huo unaanzia mwaka 2019 hadi 2024 na unakwenda kujibu matatizo yatokanayo na uzazi ambapo maeneo 14 yamepewa kipaumbele.

Akizindua mkakati huo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dokta Binilith Mahenge amesema vifo vitokanavyo na uzazi ni janga kubwa na kutokana na hali hiyo mkoa kwa kushirikiana na wadau wa afya wameandaa mkakati huo ili kuhakikisha hakuna kifo kitokanacho na uzazi.