Sababu Za Kuwashwa Baada Ya Kuoga


Wataalamu wa afya ya ngozi pia wanabainisha kuwa kuoga muda mrefu na mara kwa mara, matumizi ya sabuni zenye harufu kali na povu jingi ni mambo mengine yanayochangia kutokea kwa mzio pamoja na ukavu wa ngozi kutokana na uwezo wake wa kuondosha kiasi kikubwa cha mafuta yanayolinda ngozi.

Ili kupunguza hali ya muwasho, “Tumia sabuni zenye mafuta, lakini zisiwe na marashi makali.”

Katika hali ya kawaida kitendo cha kuoga kinapaswa kuchukuliwa kama jambo la kufurahisha kutokana na ukweli kwamba huufanya mwili uburudike na kuwa safi. Lakini kwa baadhi ya watu mambo ni tofauti. Kuoga huwa sawa na karaha.

Moja ya matatizo ya kiafya ambayo yanayosumbua watu wengi duniani na kuwanyima raha ya maisha, ni tatizo la mwili kuwasha mara baada ya kuoga. Muwasho baada ya kuoga unaweza kujitokeza mwili mzima au unaweza kuhusisha baadhi ya sehemu.

Hali hii inaweza kuwa inajitokeza kwa muda wa dakika chache au inaweza kuchukua muda mrefu na kwa baadhi ya watu, hili linaweza kuwa tatizo sugu. Ingawa tatizo hili la kiafya ni kama mengine, lakini baadhi ya watu kwa kukosa taarifa sahihi, hulihusisha na imani potofu.

Ukweli wa mambo ni kwamba kuna sababu nyingi zinazochochea kutokea kwa tatizo hili na baadhi hazina madhara makubwa kama vile kuhatarisha kwa maisha.

Pamoja na ukweli wa kisayansi kwamba asilimia 70 ya mwili wa binadamu ni maji, kwa upande mwingine yanaweza kuwa chanzo cha matatizo ya kiafya hasa pale yanapokuwa na vitu vinavyosisimua mwili au kuchochea hali ya kutokea kwa mzio. Siyo jambo la kushangaza kuona kuwa maji ambayo ni safi na salama kwa kunywa yanaweza kuwa siyo salama kwa kuoga.

SABABU ZA MUWASHO MWILINI
Miongoni mwa sababu za kutokea kwa muwasho wa mwili baada ya kuoga ni za kimazingira na sababu zingine zinahusiana na hitilafu za urithi wa vinasaba vya kijenetiki katika mfumo wa kinga ya mwili wa mhusika.

Wakati mwingine tatizo hili linaweza kuwa ni dalili muhimu inayoonyesha baadhi ya magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza kama vile matatizo ya figo, ini, tezi shingo, matatizo ya mfumo wa damu, kisukari, saratani ya mitoki na msongo wa mawazo.

Baadhi ya tafiti zinabainisha kuwa sababu nyingine ni pamoja na uchafuzi wa mazingira ya hewa kwa kemikali zenye sumu zinazopatikana katika moshi wa tumbaku, mifuko ya plastiki, dawa za kufanyia usafi majumbani, dawa za kuua wadudu, vumbi ya ndani ya nyumba yanayobeba vimelea vya magonjwa pamoja na uchafuzi wa hewa kwa moshi wa magari na ule unaozalishwa na viwanda katika maeneo ya mijini.

Vitu hivi huufanya mwili kuathirika na kutengeneza mazingira ya ndani ambayo yanachochea kutokea kwa muwasho pindi mwili unapopata msisimuko, hali ambayo hujulikana kama mzio.

Mzio huanza pale mfumo wa kingamwili unapobainisha kemikali hizi kama mvamizi wa mwili  na kuamuru askari wake wajulikanao kama seli za T-lymphocites na B-lymphocytes kujibu mapigo ya wavamizi kwa kuzalisha kemikali maalumu zijulikanazo kama immunoglobulin E na prostaglandins ambazo husababisha kuzalishwa kwa kemikali nyingine kama vile histamine, tryptase na  chymase, kwa lengo la kuvunja nguvu za kemikali vamizi.

NI KWA NAMNA GANI?
Baadhi ya watafiti wanabainisha kuwa kutokana na hitilafu za vinasaba vya kijenetiki kunakuwa na ongezeko la kemikali aina ya Cyclic Adenosine Monophosphate  Phosphodiesterase ambayo inaharibu mfumo wa udhibiti wa seli za kinga mwili aina ya basophils na  seli za mast  na kusababisha zisisimuke kupita kiasi na kuzalisha histamine nyingi ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa mzio.

Watu wengi wana mzio wa vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na dawa za tiba, kemikali zinazotumika kutengenezea sabuni, vipodozi, aina fulani za vyakula, kemikali kadhaa zinazotumika katika usindikaji wa vyakula, kemikali zinazowekwa katika maji kama vile chlorine (watergurd), maji ya kuoga yenye chumvi nyingi na kemikali zinazotumika katika utengenezaji wa nguo, ikiwa ni pamoja na mataulo ya kuogea.

Mapambano kati ya kinga mwili na kile ambacho mwili hukibainisha kwa makosa kama wavamizi, yanaweza kusababisha magonjwa ya pumu, muwasho wa ngozi, muwasho wa macho, mafua ya mara kwa mara na maumivu ya tumbo.

SABABU NYINGINE
Mapambano haya pia yanaweza kusababisha hali ya mzio dhidi ya vyakula kama vile mayai, maziwa, samaki, nyama, karanga, vyakula vitokanavyo na unga wa ngano, kahawa, pombe na baadhi ya vyakula na vinywaji vinavyotengenezwa au kusindikwa viwandani kwa kutumia kemikali. Hali hii pia inaweza kutokea kutokana na kula vyakula vyenye mchanganyiko wa vikolezo kama pilau na viungo vingi.

Ulaji wa vyakula vyenye upungufu wa viinilishe nao unatajwa kuwa unachangia kutokea kwa tatizo la mwili kuwasha wakati wa kuoga.
Watu wengi hawatumii kiasi cha kutosha cha matunda, mboga na mafuta salama yanayotokana na mimea au samaki, jambo ambalo huathiri vibaya afya ya ngozi.

Tatizo jingine linalochangia mwili kuwasha wakati wa kuoga ni kutokutumia kiasi cha kutosha cha maji ya kunywa kila siku. Hali hiyo inafanya mwili kuwa na upungufu wa maji na kuathiri vibaya afya ya ngozi na uwezo wake wa kuondosha sumu mwilini.

Ngozi isiyokuwa na afya njema inashindwa kutunza kiasi cha kutosha cha unyevu na kusababisha ukavu. Ngozi inapokuwa kavu husisimka kupita kiasi wakati wa kuoga na kusababisha muwasho. Sababu ya mwili kuwasha baada ya kuoga ni kuishi katika hali ya msongo wa mawazo inayosababishwa na hofu, wasiwasi na sonona.

Tatizo jingine linalosisimua mwili na kusababisha muwasho wakati wa kuoga ni kujisugua kupita kiasi au kujisugua wakati wa kujifuta kwa taulo baada ya kuoga.  Kwa kawaida seli za ngozi zilizokufa, jasho na vumbi ndivyo vinasababisha mwili kuchafuka.

Lakini uchafu huo huondoka mwilini tunapooga na nguvu nyingi hazihitajiki ili kuondosha uchafu na taka mwili juu ya ngozi. Matumizi ya nguvu nyingi na kusugua ngozi sana, husababisha madhara kwenye ngozi na kusababisha muwasho au ukavu wa ngozi kwa kuondosha mafuta yanayolinda usalama wa ngozi.

Watu wenye tatizo hili wanaweza kufanya mazoezi mepesi kabla ya kuoga ili kupasha mwili joto au kupaka lotion ili kuifanya ngozi kuwa na unyevu na kupunguza hali ya ukavu wa ngozi.