TBS yatoa Elimu kwa zaidi ya Wanawake na vijana 800


Zaidi ya wanawake na vijana 800 katika Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, wameelimishwa jinsi Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linavyotekeleza majukumu mapya ambayo awali yalikuwa chini ya iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).

Wananchi hao walipatiwa elimu hiyo kupitia kongamano la siku mbili lililoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kwa kushirikiana na wilaya na kudhaminiwa na TBS. Kongamano hilo la siku mbili lilianza Septemba 4 na kumalizika Septemba 5, mwaka huu.

Akitoa elimu kwa washiriki wa kongamano hilo kuhusiana na mabadiliko hayo, Ofisa Uhusiano wa TBS, Neema Mtemvu, alisema TBS inatekeleza majukumu hayo kufuatia mabadiliko ya sheria ya fedha ya mwaka 2019 ambayo yameleta mabadiliko katika sheria ya viwango Na: 2 ya mwaka 2009.

Kutokana na mabadiliko hayo, Mtemvu alisema majukumu ya kudhibiti ubora na usalama wa chakula na vipodozi yanafanywa na TBS.

Alitaja huduma zinazotolewa na shirika hilo kwa sasa kuwa ni pamoja na usajili wa jengo,  kusimamia masuala ya usalama na ubora wa chakula na vipondozi na upimaji wa bidhaa za vyakula na vipodozi kwa lengo la kudhibiti ubora.

Majukumu mengine ni utoaji wa leseni au cheti cha TBS kwa bidhaa za chakula na vipodozi na usajili wa bidhaa za vyakula na vipodozi vinavyotoka nje ya nchi.

Wakati huo huo, maofisa wa shirika hilo walitoa elimu ya viwango kwa washiriki wa kongamano hilo miongoni mwao wakiwa ni wajasiriamali.

Akizungumza wakati wa kutoa mafunzo hayo kupitia kongamano hilo,  Mtemvu, alitoa wito kwa wajasiriamali kutumia fursa ya huduma ya bure ya kuthibitisha ubora wa bidhaa zao ambayo inatolewa na shirika hilo ili kuwainua wajasiriamali na hatimaye kuweza kushindana na kuuza bidhaa zao katika masoko ya ndani na nje ya nchi bila vikwazo vya kibiashara.

Alisema kinachotakiwa ni mjasiriamali kupata barua ya utambulisho kutoka Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) na akiipeleka TBS mchakato wa kumthibitishia ubora bidhaa zake unaanza mara moja.

Alitoa wito kwa washiriki wa kongamano hilo kutumia elimu waliyoipata kujitokeza TBS kuthibitisha ubora wa bidhaa zao na kuwa mabalozi wazuri wa masuala ya viwango.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ali Hapi, alitoa wito kwa wajasiriamali kujiajiri na hatimaye kuwa wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda vikubwa, hivyo kusaidia kutoa ajira kwa Watanzania.

Hapi alifafanua kwamba Serikali peke yake haiwezi kuajira kwa wananchi wote, hivyo alitoa mwito kwa washiriki wa kongamano hilo kuchangamkia fursa za kujiajiri.