TCRA Kanda ya Kaskazini yasisitiza usajili wa simu kwa alama za vidole ni bure



Na John Walter-Babari-Manyara

Ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata mawasiliano bora bila usumbufu, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Kaskazini ikishirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), imeendelea na zoezi la kutoa elimu ya usajili mpya wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole mkoani Manyara.

Mamlaka hiyo imetoa angalizo kwa wananchi na makampuni ya simu za Mikononi kuwa zoezi hilo la usajili wa alama za Vidole ni bure kwa mtu yeyote hivyo wasikubali kutoa malipo yeyote.

Akitoa huduma eneo la stendi ya zamani mjini Babati, Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano kanda ya Kaskazini Mhandisi Imelda Salum, amesema kuwa usajili huo ni usalama kwa mtumiaji wa mawasiliano ambapo kwa alama hizo hawawezi kuingiliana na mtu mwingine yeyote duniani.


Amesema kuwa lengo la kuendesha zoezi la usajili wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole ni kudhibiti vitendo vya uhalifu unaofanywa kwa njia ya mitandao ukiwepo utapeli hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kusajili laini zao za simu .

Sambamba na hayo amewahasa wananchi wa Babati kutumia namba zao za simu  kwa uangalifu ili kuepuka mawasiliano yao kutumiwa vibaya na wahalifu.

Ameongeza kuwa  wapo Mjini Babati katika eneo la stendi ya zamani kwa siku tatu yaani Jumatano,Alhamisi na Ijumaa ili kutoa elimu mbalimbali zinazohusu Mawasiliano bila gharama yeyote huku wakitoa vitabu vinavyotoa maelezo mbalimbali juu ya TCRA.

 Pia Tcra inawasaidia wananchi waliojiandikisha, kupata kitambulisho cha Taifa  kupata namba ya kitambulisho ili kuendelea na usajili wa laini zao za simu wakati wanasubiri kitambulisho hicho kukamilika.

Nae Afisa Usajili wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Mkoa wa Manyara, Emmanuel Joshua amesema zoezi hilo la serikali limelenga kuhakikisha kila Mmoja anakuwa na namba ya simu inayotambulika na kwamba itasaidia kupunguza vitendo vya kitapeli kwa njia ya simu.

Nao baadhi ya wakazi wa mji wa Babati waliojitokeza katika zoezi hilo wameieleza Muungwana Blog kuwa  zoezi hilo la usajili wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole litasaidia kuepukana na vitendo vya utapeli kwa njia ya mitandao ambavyo wengi  wamekuwa wakikumbana navyo.

Ikumbukwe kwamba seriakli  imeshawatangazia wananchi juu ya usajili wa namba za simu kwa alama za vidole tangu Mei 1 mwaka huu, hivyo ni vyema wasajili kwani baada ya zoezi hilo kukamilika Desemaba 31 2019 ,namba za simu ambazo hazijasajiliwa zitafungwa na watoa huduma.

Baada ya TCRA kutoa Elimu kwa wakazi wa Babati, watendelea  katika wilaya ya Hanang kisha Mbulu.