Vitunguu swaumu vyapata soko kwenye nchi Tisa


Mkakati wa Serikali kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania nje unaendelea kuzaa matunda ambapo kwa sasa vitunguu swaumu vimepata soko kwenye nchi tisa. Ilielezwa bungeni kuwa vinauzwa vikiwa ghafi.

Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba aliyesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Massay (CCM) aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kutafuta soko la vitunguu swaumu nje ya nchi.

"Vitunguu swaumu vinauzwa katika nchi ya Shelisheli, visiwa vya Comoro, Msumbiji, Zambia, Mauritania, Kenya, Uganda na Falme za Kiarabu," alisema.

Mgumba alisema katika kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao ya kilimo vikiwemo vitunguu swaumu, serikali imekamilisha upatikanaji wa simbomilia (barcode)pamoja na kubainisha viwango vya ubora kwa kulitumia Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Aidha, wizara imeanzisha kitengo cha masoko chenye jukumu la kuyatafuta ndani na nje ya nchi ikiwemo ya vitunguu swaumu.

Hayo yote yanafanyika ili kuwa na taarifa sahihi za kuwapa wakulima waweze kuzalisha mazao yanayokidhi mahitaji ya soko.

Alisema, serikali kupitia Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) ilivijengea uwezo vikundi vya wakulima katika bonde la Bashay na kuviwezesha kusindika vitunguu swaumu.

Jitihada hizo zimesaidia kuongeza thamani ya zao la vitunguu swaumu, muda wa kuvihifadhi bila kuharibika na kuimarisha soko la bidhaa hiyo ndani na nje ya nchi," alisema.