Vurugu zaibuka mjini Hong Kong

Wafuasi wa maandamano yanayoendelea mjini Hong Kong ya kudai mageuzi ya kidemokrasia wamekabiliana na wafuasi wanaoiunga mkono serikali ya China katika eneo moja la maduka katika jimbo hilo lenye utawala wa ndani.

Mamia ya waandamanaji waliojazana katika uwanja wa Amoy Plazza wilayani Kowloon, walipeperusha bendera za China na kuisifu nchi hiyo kabla ya waandamanaji wengine nao kukusanyika katika eneo hilo hilo na kuanza kushambuliana.

Hatua hiyo ilizusha vurugu huku baadhi ya wafuasi wa pande zote mbili wakirushiana ngumi na wengine wakitumia mianvuli kuwapiga wapinzani wao.

Polisi baadae walifika katika eneo hilo na kudhibiti hali huku watu kadhaa wakikamatwa. Mapigano hayo yanatokea baada ya maandamano ya mwezi mmoja sasa ya kudai demokrasia zaidi katika mjini huo unaotawaliwa na China.