Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza aomba msamaha kwa mgawanyiko uliopo

Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza aliyeitisha kura ya maoni juu ya suala la nchi hiyo kujiondoa katika Umoja wa Ulaya maarufu kama Brexit, ameomba msamaha kwa mgawanyiko ulioleta.

Akizungumza na gazeti la Times nchini humo, David Cameron amesema katika mahojiano yaliyochapishwa hii leo kwamba anafikiria matokeo ya kura hiyo ya maoni kila siku na ana wasiwasi juu ya kile kitakachofuata.

Cameron, aliyeunga mkono Uingereza kubakia katika Umoja wa Ulaya , alijiuzulu baada ya kukamilika kwa kura hiyo ya maoni mwaka 2016.

Kiongozi huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 52 alimshambulia mshirika wake wa zamani Boris Johnson ambaye ni Waziri Mkuu wa sasa wa Uingereza pamoja na Waziri wa Mazingira Michael Gove kwa kuendesha kampeni ya Uingereza kuondoka katika Umoja wa Ulaya.