Na Ahmad Mmow, Nachingwea.
Wahitimu wa mafunzo ya jeshi kwa mujibu wa sheria katika kikosi cha Jeshi namba 843 (843KJ) cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kilichopo wilayani na Nachingewa, mkoani Lindi licha ya kuishukuru na kipongeza serikali, lakini wameiomba iongeze muda wa mafunzo.
Pongezi na ombi hilo kwa serikali zilitolewa juzi na wahitimu wa mafunzo katika kikosi namba 843 kwa mujibu wa sharia kupitia operesheni makao makuu Dodoma. Ambayo yalifungwa juzi kikosini hapo.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi wakati wa hafla ya ufungaji mafunzo hayo, mmoja wa wahitimu hao, Katherine Parsalau alisema serikali imefanya jambo jema kurejesha utaratibu wahitimu wa kidato cha sita kujiunga na JKT kupata mafunzo. Hata hivyo kutokana na umuhimu na faida ya mafunzo hayo, muda wa miezi mitatu hautoshi.
Alisema serikali hainabudi kushukuriwa na kupongezwa kwa uamuzi huo. Kwani mafunzo hayo yanaumuhimu mkubwa kwa vijana ili wawe wazalendo kwa taifa lao, waadilifu na waaminifu. Lakini pia mafunzo hayo yanaweza kuwa ni njia ya kuwaandaa viongozi wenye sifa hizo.
Mhitimu huyo ambae alisoma risala hiyo kwaniaba ya wahitimu wenzake 1,001, alisema kutokana na umuhimu na faida hizo serikali iangalie uwezekano wa kuongeza muda wa mafunzo badala ya miezi mitatu yawe ya miezi sita au mwaka mmoja.
" Tunaiomba serikali iangalie uwezekano wakuongeza muda wa mafunzo. Kwani yanasaidia kuwaandaa vijana wanaoweza kuwa viongozi wazalendo, watiifu na waaminifu kwa nchi," alisisitiza Katherine.
Aidha muhitimu huyo alitoa wito kwa vijana wenye sifa za kujiunga na jeshi hilo wasisite kujiunga, kwani vijana wengi wenye sifa za kujiunga hawafanyi hivyo. Hali ambayo inakwamisha nia njema ya serikali kwa vijana hao.
Mafunzo hayo yaliyofungwa juzi yalikuwa na wahitimu 1002 ambao wamefanikiwa kumaliza miongoni mwa 1,042 waliojiunga na kuripoti katika kambi hiyo. Huku 40 wakishindwa kumaliza kutokana na sababu mbalimbali.
