Waziri Kairuki agawa taulo za Kike kwa Wanafunzi Same


Na Ferdinand Shayo, Killimanjaro

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Angellah Kairuki amegawa taulo za kike kwa wanafunzi wa shule ya sekondari mkombozi iliyoko kijiji cha  Hedaru wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro lengo ikiwa ni kuwawezesha wasichana kusoma bila usumbufu wanapokuwa katika kipindi cha hedhi.


Kairuki alifika shuleni hapo na kuzungumza na wanafunzi wa kike huku akiwataka kujiepusha na vishawishi pamoja na tamaa ili waweze kutimiza ndoto zao na kusaidia jamii inayowazunguka.

Aidha amesema kuwa ataendelea kushirikiana na shule hiyo katika kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa uzio ,uhaba wa matundu ya vyoo ili wanafnzi hao waweze kusoma katika mazingira rafiki.

Mkuu wa shule ya Sekondari ya Mkombozi, Furahini Lubuwa hiyo amempongeza Waziri  Kairuki kwa kutembelea wanafunzi hao na kuwapatia msaada wa taulo za kike kwani zitawasaidia hasa wale ambao wanatoka katika familia zenye kipato cha chini .

Mmoja wa Wanafunzi wa Shule hiyo, Fatuma Hemed amesema kuwa msaada huo utawawezesha kusoma bila usumbufu kwani wapofikia kipindi cha hedhi huwa na hofu hasa wale ambao hawawezi kujisitiri vyema hivyo msaada huo utawasaidia.