Agizo la Waziri Lugola la kupunguza pikipiki kituoni polisi latekelezwa Tarime/Rorya



Na Timothy Itembe Mara.

Waendesha Pikipiki mkoa wa kipolisi Tarime/Rorya wamelishukuru jeshi la polisi kutekeleza Agizo la Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi Kangi Lugola la kilitaka jeshi hilo kuacha tabia ya kukamata pikipiki  kwa makosa madogomadogo huku wakizipeleka kituoni polisi.

Akitoa shukurani hizo kwa niaba ya wenzake,Amosi Mang'era mmoja wa waendesha pikipiki alisema kuwa tangu Waziri wa mambo ya ndani ya Nchi Kangi Lugola atoe agizo la polisi kuacha tabia ya kukamata pikipiki kwa makosa madogo madogo na kuzipeleka kituoni,polisi wameacha tabia hiyo badala yake sasa wanakamata pikipiki zenye makosa yaliyoelekezwa na waziri.

Mang'era aliongeza kuwa polisi wa usalama barabarani kwa mkoa wa kipolisi Tarime/Rorya kwasasa hawafukuzani na waendesha pikipiki barabarani badala yake wanafanya kazi yao  kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.

mkuu wa kikosi cha usalama barabarani Mrakibu wa jeshi la polisi Tarime/Rorya,SP,Ally Shaali  alisema kuwa kupungua kwa pikipiki zinazokamatwa kwa makosa ya usalama barabarani kumetokana na waendesha pikipiki kuwa na uelewa wa vyombo vya moto na matumizi sahihi ambayo yanatokana na elimu inayotolewa na kwa watumiaji wa vyombo vya moto.

"Niwatake waendesha pikipiki maarufu kama Bodaboda kufuata kanuni,taratibu na sheria za usalama barabarani zinazoendelea na jeshi la polisi ambazo zinatolewa kila wakati  ili kuweza kufanya kazi hiyo inayowaingizia kipato kwa Amani kwani biashara ya Bodaboda ni biashara kama biashara nyingine hivyo waendesha pikipiki wanatakiwa kuheshimu biashara yao ili waweze kusonga mbele kimaisha na kujiingizia kipato kikubwa"alisema Shaali.

SP huyo aliongeza kusisitiza kuwa waendesha pikipiki waepuke makosa yanayotokana na  kukamatwa kwao kama vile  kutovaa kofia ngumu,kubeba abiria zaidi ya mmoja kwenye pikipiki,kuegesha sehemu isiyoruhusiwa kwenye kona,kuendesha pikipiki katika hali ya ulevi,kuendesha pikipiki mbovu,kutokuwa na leseni ya udereva na Bima ya pikipiki.