Akamatwa na Polisi kwa kujiandikisha mara mbili kwenye daftari la Wapiga Kura


Mkazi wa Kasanga Manispaa ya Morogoro, Ngeze Mwagilo (29) anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kujiandikisha mara mbili katika daftari la wapigakura kwenye vituo viwili tofauti ndani ya manispaa ya Morogoro.

Akizungumza na Waandishi wa Habari hapo jana Kamanda wa polisi mkoani Morogoro, Wilibroad Mutafungwa alisema kuwa mtu alikamatwa baada ya jeshi hilo kupata taarifa na kumfuatilia mtuhumiwa huyo wakati wa shughuli ya uandikishaji ikiendelea.

Mtuhumiwa huyo anadaiwa kujiandikisha katika kituo cha Kasanga kata ya Mindu na baadaye kwenda kujiandikisha katika kituo cha kiwanja cha Ndege kata ya Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro.

Ameongeza kuwa mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa na atafikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika ili sheria ichukue mkondo wake.

Mutafungwa amewatahadharisha wananchi mkoani humo wenye lengo la kutaka kuvuruga shughuli hiyo watachukuliwa hatua za kisheria kuwa polisi itahakikisha inawakamata huku akiwataka kuacha kufanya uhalifu huo.