Na Amiri kilagalila-Njombe
Mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka ameagiza halmashauri zote 6 za mkoa wa Njombe kuhakikisha zinajiuliza zimefikia asilimia ngapi ili kufikia lengo la kitaifa la 50% la kaya zote kujiunga na mfuko wa afya ya jamii (CHF) ifikapo septemba 2020.
Ole Sendeka ametoa agizo hilo akiwa katika kikao cha hamasa na uzinduzi wa mfuko wa afya ya jamii ulioboreshwa kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Njombe mkoani hapo.
“Tuna nia ya kuhakikisha tunajenga uelewa na kufanya uhamasishaji wa jamii kujiunga na mfuko huu ili kufikia lengo la kitaifa la 50% la kaya zote kujiunga na mfuko wa afya ya jamii ifikapo septemba 2020,kila halmashauri ijiulize kama tunatakiwa kufika lengo la asilimia 50,halmashauri yak oleo imefikia asilimia ngapi”alisema Ole Sendeka
Aidha amewataka viongozi mbali mbali wa serikali na dini kutumia fursa ya kutoa elimu na uhamasishaji kwa wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya jamii ulioboreshwa ili kuwasaidia wananchi kupata huduma ya afya kwa fedha kidogo.
Mratibu wa mfuko wa afya ya jamii (CHF) mkoa wa Njombe Erick Haule amesema mkoa wa Njombe una jumla ya kaya 27,097 sawa na asilimia 16% zilizojiunga katika mfuko wa CHF.
“Kaya zilizojiunga katika mfuko wa CHF bado ni kidogo sana ambayo ni 16% ya kaya zote na 53% ya lengo la kitaifa la 30% ya kaya zilizopo katika mkoa,hii ni kulingana na kaya zilizojiunga na mfuko wa afya ya jamii unaoendelea ambao kwa sasa uandikishaji wake umefikia kikomo na utekelezaji wake utakoma juni 20120”alisema Haule
Aidha amesema mkoa ulianza uandikishaji wa CHF iliyoboreshwa mwishoni mwa mwezi Agosti,2019 ambapo halmashauri nne zilianza uandikishaji mpaka sept,2019 huku ludewa Dc ikifikia kaya 775,Njombe DC kaya 65,Makambako TC kaya 91 na Njombe mji kaya 38 ambayo jumla ya kaya zote ni 969 hivyo kasi ya uandikishaji bado si ya kuridhisha.
Sada Msangi na Rajab Msigwa ni baadhi ya wakazi wa mkoa wa Njombe wanasema maboresho hayo yatawasaidia kupata matibabu sehemu nyingi za kutolea huduma ukilinganisha na awali.
Jumla ya watu sita katika kaya kupatiwa huduma ya matibabu kupitia CHF kwa shilingi 30,000 kwa mwaka katika zahanati,kituo cha afya,hospitali ya wilaya na hospitali ya rufaa ya mkoa.


