Hatua muhimu za kufanikiwa katika maisha



kwenye kipengele cha kuchagua marafiki wema katika njia yako ya kusaka mafanikio maishani. Nikasema hutakiwa kuambatana na marafiki ambao hakika kazi yao kubwa ni kukuvunja moyo. Hupaswi kabisa. Siku zote chagua watu ambao watakutia moyo na kukuongezea maarifa katika safari yako ya kutimiza hizo ndoto kubwa unazoota.

Siku zote mafanikio ni mipango, ndiyo maana hapa nasisitiza kupanga mambo makubwa maishani mwako ili upate mafanikio makubwa pia. Wengi huishia kuwaza na kujipangia ndoto ndogo ndiyo maana hata mafanikio yao yanabaki kuwa madogo na ya kawaida sana.

Katika kipengele hiki wengi sana hushindwa kutimiza hayo. Hudhani kukaa mbali na watu waliowazoea ni hatari na hawawezi kufurahia maisha jambo ambalo halina ukweli hata kidogo. Chagua marafiki wapya, achana kabisa na watu ambao wanakuvunja moyo kila hatua unayoichukua maishani mwako.

Msomaji wangu, hakuna kitu kibaya maishani kama kuakatishwa tamaa katika kipindi ambacho unajiwekea malengo mazuri. Elewa kuwa bila hao uliowazoea maisha yatasonga mbele  tena kwa furaha. Wakati mwingine huwa ni busara sana kuachana na watu ambao hawana faida yoyote maishani mwetu. Narudia tena kuwa, kaa na jitenge mbali sana na watu wavunja moyo. Hawana maana yoyote.

Jifunze kwa waliofanikiwa.
Hiki ni kipengele muhimu cha mwisho katika makala haya. Siku zote kila unachokifanya, lazima kuna watu waliokifanikisha hapo kabla. Jiweke nao karibu ili ujifunze ni kwa namna gani waliweza kufanikisha malengo yao makubwa kama unayoyaota.

Ninaposema kukutana na waliofanikiwa sina maana uanze harakati za kwenda Marekani ukaonane na Warren Buffet au Bill Gates, la hasha! Unaweza kukutana na watu hawa kwenye mawazo yako. Namaanisha kusoma vitabu walivyoandika kuhusu maisha na mafanikio.

Tatizo kubwa tulilonalo Watanzania wengi ni tabia ya kutopendelea kusoma vitabu. Ndugu zangu, maarifa na mbinu nyingi za mafanikio maishani zimo kwenye vitabu. Nasema hivyo kwa sababu mtu anapoandika kitabu, hutoa mawazo yake yote kwa utulivu wa hali ya juu tofauti na anayezungumza kwa mdomo.

Kwa maana nyingine ni kwamba kwenye vitabu kuna maarifa na elimu kubwa mno kuhusu mafanikio maishani.

Jiwekee utaratibu wa kusoma vitabu. Binafsi nilipoamua kuanza safari hii ndefu ya kutafuta mafanikio maishani, niliamua kujielimisha kwa kusoma vitabu. Hadi sasa nimesoma vitabu vingi mno.

Kuna wakati nilikuwa nasoma vitabu hadi ndugu zangu wakawa wananiambia nakaribia kuwehuka! Niliamini katika kujielimisha, hata sasa ninapoandika makala haya, chumbani kwangu kuna maktaba iliyojaa vitabu vingi mno.

Kuna vitabu vya akina Napoleon Hill, Dk. Norman Vincent Peal, Robert T. Kiyosaki, Donald Trump, Willie Jollie, Harry Rollein, Babra De Angelis, Les Brown, Mahtma Gandh na wengineo kibao, hawa ni watu maarufu duniani walioandika vitabu vingi vya kupata mafanikio maishani. Tafuta maarifa. Waza makubwa, pambana na maisha yanawezekana.