Manispaa ya Lindi yaonesha udhibiti wa matumizi ya fedha za ujenzi wa kituo cha Afya



Na Ahmad Mmow, Lindi.

Halmashauri ya manispaa ya Lindi imeonesha kwa vitendo kuunga mkono jitihada za Rais Dkt John Magufuli za kuepuka matumizi ya fedha yasiyo ya lazima na kuonesha matumizi sahihi na thamani ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Hayo yamebainishwa kwenye taarifa ya ujenzi wa kituo cha utoaji huduma katika kituo cha Afya cha Mnazimmoja, manispaa ya Lindi, iliyosomwa na kaimu mganga mkuu wa hospitali ya manispaa ya Lindi, Abilahi Mbingu kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa wa mwaka 2019, Mzee Mkongea Ali katika mtaa wa Mnazimmoja.

Mbingu alisema  kwakutumia mfumo wa ushirikishaji wananchi katika ujenzi wa miradi ya maendeleo(force account) wamefanikiwa kujenga  jengo la akinamama(maternity), jengo la upasuaji(theatre),jengo la kuhifadhia maiti(mortuary), nyumba tatu za watumishi(staff houses),jengo la utawala( adminstration block) wagonjwa wa nje(out partient deparment), jengo la kusafishha nguo(laundry) na kuchomea taka. Hatahivyo wamefanikiwa kujenga miundombinu ya ziada kwakutumia fedha zilizotengwa kwa kazi za msingi zilizokadiriwa kutumia fedha hizo.

'' Kutokana na utendaji mzuri wa kamati, tulifanikiwa kujenga miundombinu ya ziada kwa fedha zilezile . Kazi za ziada zilizofanyika ni ujenzi wa mifumo ya maji taka, ujenzi wa uzio, ujenzi wa korido moja na kuweka mfumo wa utoaji huduma za afya,'' alisema Mbingu

Mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Mnazimmoja ulianza rasmi mwezi Februari 2018, baada ya Serikali kuona umuhimu wa kuboresha huduma zinazotolewa katika vituo vya afya nchini.

Mradi huo umegharimu shilingi 1,115,500,000. Kati ya hizo, shilingi 1,100,000,000 zimetolewa na serikali kuu, 11,000,000 zimetolewa na halmashauri na 4,500,000 ni nguvu za wananchi.