Na. Ezekiel Mtonyole, Dodoma
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imetoa hali ya mfumuko wa Bei kwa mwezi unaoishia Mwezi wa tisa huku takwimu zikionesha kuwa mfumuko wa bei umeshuka kwa asilimia 0.2, kutoka asilimia 3.6 kwa mwezi wa nane, na kufikia asilimia 3.4 kwa mwezi wa tisa 2019.
Akitangaza takwimu hizo ofisini kwake Jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Sensa ya watu na takwimu za Jamii, Ruth Davison, amesema kushuka kwa mfumuko wa bei umechangiwa na kupungua kwa bei zisizokuwa za vyakula baadhi zikiwa ni mafuta ya taa, Petrol, majiko ya gesi.
"Mfumuko wa bei kwa mwezi Septemba umepungua kwa asilimia 0.2, kutoka asilimia 3.6 kwa August, hadi kufikia 3.4 kwa mwezi Septemba, baadhi ya bidhaa zisizokuwa za vyakula zilizochangia kushika kwa bei."
"Baadhi ya bidhaa zisizokuwa za vyakula zilizopunguza bei kwa mwezi Septemba 2019, zikilinganishwa na bei za Septemba 2018, ni Mafuta ya taa 1.0%, Petrol 3.3%, Majiko ya gesi 1.5%, Dawa za kuulia wadudu nyumbani 2.2%na Mafuta ya nywele1.3%" amesema Ruth.
Aidha amebainisha kuwa mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba 2019, umeongezeka hadi kufikia asilimia 4.0 kutoka asilimia 3.7 kwa mwaka ulioishia mwezi Agost, 2019.
Kwa upande wa Nchi jirani za Kenya na Uganda, kwa upande wa Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Septemba, 2019 umepungua kutoka asilimia 5.00 kwa mwaka ulioishia mwezi Agost hadi kufikia asilimia 3.83, na Uganda umepungua kutoka 2.1 hadi kufikia 1.9 kwa mwezi Septemba.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa sheria ya Takwimu ya mwaka 2015, pamoja na mapitio yake 2018, NBS imepewa Mamlaka ya kutoa na kusimamia na kuratibu upatikanaji wa taarifa za Takwimu hapa Nchini.
