Mkutano wa ufadhili wa Malaria, TB na AIDS wafunguliwa Ufaransa

Wakfu wa kimataifa unaofadhili mapambano dhidi ya magonjwa matatu makubwa ya Malaria, kifua Kikuu na Ukimwi unatarajia kukusanya dola bilioni 14 katika mkutano wa ufadhili huko Lyon, Ufaransa.

Wakfu huo wa Global Fund to Fight Aids ulioandaa mkutano huo unaofunguliwa hii leo umesema iwapo malengo yake yatafikiwa utaweza kunusuru maisha ya watu milioni 16 na kuzuia maambukizi milioni 234 ifikapo mwaka 2023.

Wakfu huo ambao kwa kiasi kikubwa hufadhiliwa na serikali na watu binafsi uliahidiwa dola bilioni 12.9 wakati wa mkutano wake wa mwisho huko Canada mwaka 2016.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anatarajiwa kuhudhuria kesho Alhamisi na huenda akaungana na viongozi wengine 10 ama zaidi wa dunia.

Kulingana na wakfu huo asilimia 72 ya fedha zilizotumika tangu mwaka 2016 zilipelekwa Afrika na asilimia 20 ilitumika Asia na eneo la Pacific.