Rais Lenin Moreno atangaza sheria ya kutotembea usiku


Rais wa Ecuador Lenin Moreno ametangaza sheria ya kutotembea usiku katika maeneo na majengo nyeti baada waandamanaji wanaoipinga serikali kuvamia jengo la bunge.

Sheria hiyo iliyoanza kutekelezwa jana kuanzia saa mbili usiku hadi saa 11 alfajiri itatekelezwa hadi Jumapili. Sheria hiyo inatekelezwa wakati ambapo tayari rais Moreno ametangaza hali ya dharura Alhamisi iliyopita.

Kulingana na gazeti la La Hora dharura hiyo itadumu kwa siku 30, badala ya 60 kufuatia uamuzi wa mahakama ya katiba.

Waziri wa mambo ya ndani Maria Paula Romo alisema mapema jana waandamanaji hao walilivamia jengo la bunge kabla ya kufurushwa na polisi, na watu 169 kati ya waandamanaji 10,000 walikamatwa.

Maandamano hayo ya siku sita yanafuatia kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta na hatua kali za kiuchumi.