RC Ole Sendeka aona umuhimu wa wanafunzi wote kupitia Skauti


Na Amiri kilagalila-Njombe

Mkuu wa mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka amebariki kuweka kipaumbele shule zote za msingi na sekondari mkoani humo, kuhakikisha asilimia 100 ya wanafunzi waweze kuhudhuria na kujiunga mafunzo ya Skauti ili kuimarisha uzalendo wa vijana katika nchi yao.

Olesendeka ameyasema hayo mkoani Njombe akiwa katika mahafali ya vijana wa Skauti 187 wa sekondari  za mkoa wa Njombe yaliyofanyika katika ukumbi wa sekondari Mpechi mjini Njombe.

“Tunataka tuone namna ambavyo mafunzo haya na elimu hii ya skauti katika halmashauri zetu iwe ni jambo la kipaumbele katika shule zetu zote za msingi na sekondari na mimi nitashirikiana na maskauti senior tuone namna gani tutaleta hamasa tuhakikishe tunakuwa na vijana wengi wa kutosha kama sio wote asilimia mia moja waweze kuhudhuria mafunzo haya”alisema Ole Sendeka

Aidha amesema serikali mkoani Njombe ina uhakika na ukakamavu  wa vijana wa skauti na kuona haja ya kuendelea kutoa upendeleo maalumu wakati wa uchakataji wa majina ya vijana wanaokwenda kujiunga na jeshi la kujenga taifa na kuangalia rekodi yao.

Awali mkuu wa wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri aliomba  shule zote za msingi na sekondari katika wilaya ya Njombe kujiunga na Mafunzo ya Skauti.

“Nilikuwa naomba nilete ombi langu, na nimefurahi kwamba wakurugenzi wapo hapa na maafisa elimu wa msingi na sekondari, ningefurahi kama ungetafutwa utaratibu ambao shule zote ikiwezekana, kwasababu skauti ipo chini ya wizara ya elimu, ingewezekana wanafunzi wote wakawe ni Skauti”alisema Msafiri

Kamishna wa Skauti mkoa wa Njombe, Anitha Ngole amesema licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa ofisi na eneo rasmi kwa ajili ya kambi ya skauti, bado chama hicho mkoa wa Njombe kina malengo mengi huku kikiwa  kimefanikiwa kuwa na Skauti 2338 wa kiume wakiwa 1084 huku wa kike wakiwa 1254.