Wafanyabiashara wasikitishwa na miundo mbinu mibovu soko la Ngara mjini



Na George Bahemu, Ngara-Kagera.

Baadhi ya wafanya biashara wa soko kuu la Ngara mjini wilaya ya Ngara mkoani Kagera wameiomba serikali kuwaboreshea miundo mbinu katika soko lao.

Wakizungumza na Muungwana Blog wamesema kuwa wanapata changamoto wakati wa uuzaji wa bidhaa zao kwani huloa maji na kusababisha hasara hali ambayo inasababisha uchumi wao kushuka kwa kiasi kikubwa.

Wamesema soko hilo linakaribisha nchi jirani kama Burundi na Rwanda  kwani nao hufanya biashara katika soko hilo licha ya kuwa na miundo mbinu mibovu ambayo inapelekea baadhi ya bidhaa zao kama mchele na viazi kuharibika.

Angel ambaye ni mfanya biashara katika soko hilo amesema kuwa katika uuzaji wao wanapata shida kwani upepo ukivuma husababisha taka zote kujaa ndani ya soko nakuchafua  mazingira ndani ya soko hilo.

Kabla ya uchaguzi serikali ilituahidi kuwa watatujengea soko imara lakini mpaka Sasa bado halijajengwa ukiangalia wilaya zingine masoko yamejengwa vizuri sisi  bado tunahangaika "Amesema Angel."

Kwa upande wake Julius Bukobero ambaye ni Afisa mtendaji mkuu wa mamlaka ya mji mdogo Ngara amekiri kuwepo kwa tatizo hilo nakusema kuwa wahandisi wamefanya makisio ya bajeti inayotakiwa hivyo wataanza kuboresha soko hilo mwaka huu.

Hata hivyo Bukobero amewatoa wasiwasi wafanya biashara hao nakuahidi kuwa Halmashauri ya wilaya ya Ngara itawaboreshea meza, vyoo vya kisasa pamoja na miundo mbinu mingine ili waweze kufanya biashara zao bila changamoto yoyote.