Waitara aipiga jeki Hospitali Tarime


Mtoto wa Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali George Waitara, Charles Waitara ameipiga jeki Hospitali ya Wilaya ya Tarime kwa kuipa msaada wa vifaa tiba ili kuipunguzia changamoto zinazoikabili.

Kwa mujibu wa Waitara, vifaa hivyo yakiwamo magodoro 180, kompyuta tisa na mashine ya vipimo vina thamani ya Sh milioni 60. Awali wakiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Saimon Msafiri na mtangulizi wake, Charles Kabeho aliyehamishiwa wilayani Chato kwa wadhifa huo huo, walikabidhiana uongozi.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa uongozi wa hospitali ya wilaya Tarime, Waitara alisema msaada huo unatokana na huduma zinazotolewa na hospitali hiyo kuwa muhimu na msaada kwa watu wengi ndani na nje ya wilaya ya Tarime.

"Nimeguswa sana na changamoto nyingi zinazoko katika hospitali ya wilaya ya Tarime ukiwamo upungufu mkubwa wa magadoro maana hata kidogo yaliyopo yamechakaa na hata changamoto ya mashine ya vipimo vya magonjwa yakiwemo magonjwa ya ini, kisukari na figo," alisema.

Aliongeza kuwa, nilikwenda ubalozi wa China hapa nchini kuna marafiki zangu na kuandika barua ya kuwaomba msaada huo wa vifaa hivyo nao walinikubalia na kunipa hivi vifaa kwa ajili ya ndugu zangu wa Tarime na wilaya jirani wanaopata huduma katika Hospitali hii kama Rorya, Serengeti na Butiama."

Aliahidi kuendelea kutafuta misaada zaidi ikiwemo ya miundombinu ya maji ili kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli za kuwaletea wananchi maendeleo. "Nawaomba wadau wakiwemo vijana, wasomi wenzangu na wafanyabiashara kujitolea kuchangia katika kutoa misaada ya kusaidia wilaya yetu na kumuunga mkono Rais Magufuli," alisema.




Mpya zaidi Nzee zaidi